Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhalifu wa vita huwenda umefanywa na pande zote Sri Lanka

Uhalifu wa vita huwenda umefanywa na pande zote Sri Lanka

Mkuu wa Haki za Binadamu wa UM, amelaani kuongezeka idadi ya vifo na majeruhi miongoni mwa raia katika vita vikali huko Sri Lanka ya Kaskazini kati ya majeshi ya serekali na kundi la waasi.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Navi Pillay, amesema kwamba baadhi ya hatua zinazochukuliwa na jeshi la Sri Lanka na kundi la wanaotaka kujitenga la Liberation Tigers Tamil, huwenda zikawa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa, na za haki za binadamu na ubinadamu. Anasema tunahitaji kufahamu zaidi kinachoendelea, lakini tunajua vya kutosha na kwa uhakika kwamba hali ni mbaya sana. Bi Pillay anasema kuna muamko hii leo duniani, kuhusiana na hatua kama hizo, ambazo zinaweza kuchukuliwa kua ni uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Ingawa kuna maeneo yaliyootangazwa na serekali kua maeneo ya kutoshambulia kwa kuwepo raia huko Jimbo la Vanni, lakini mashambulio ya mizinga ikitokea mara kwa mara ndani ya maeneo hayo, kufuatana na habari zilizofikia ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu. Ofisi hiyo inaripoti kwamba, kuna zaidi ya watu 2 800 walouliwa na wengine elfu 7 kujeruhiwa wengi katika maeneo marufuku kushambulia tangu tarehe 20 Januari.