Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu zaidi ya 200 wauawa katika milipuko Sri Lanka, Umoja wa Mataifa na viongozi duniani walaani.

Duka la kijiji nchini Sri Lanka.
World Bank/Dominic Sansoni
Duka la kijiji nchini Sri Lanka.

Watu zaidi ya 200 wauawa katika milipuko Sri Lanka, Umoja wa Mataifa na viongozi duniani walaani.

Amani na Usalama

Zaidi ya watu 200 wameuawa na mamia kujeruhiwa kufuatia mfululizo wa wa milipuko ndani ya makanisa na hoteli kadhaa nchini Sri Lanka wakati wakristo wakijumuika kwa ajili ya misa ya kusherehekea sikukuu ya Pasaka hii leo.

 

Katika taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Antonio Guterres amesema “nimechukizwa na mashambulizi ya kigaidi” na akataka wahalifu hao “kufikishwa haraka mbele ya mkono sheria.”

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, makanisa matatu yamelengwa katika miji ya Batticaloa, Negombo na mji mkuu Colombo. Hoteli ya Shangri-La, Kingsbury,na  Cinnamon Grand zote zikiwa katika mji mkuu Colombo, zimeshambuliwa.

Hadi kufikia sasa hakuna kundi lolote ambalo limjitangaza kwa kufanya mashambulizi hayo yanayoonekana ni ya kujitolea kufa lakini inapotiwa kuwa polisi wamewakamata watu saba kuhusiana na matukio hayo.

Katibu Mkuu Guterres amenukuliwa katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake kakisema kuwa, “ilikuwa siku takatifu kwa wakristo duniani kote. Ninatuma rambirambi zangu za dhati kwa familia za waathirika, wat una serikali ya Sri Lanka na ninawatakia kupona haraka wale wote waliojeruhiwa.”

Aidha amepongeza uongozi na mshikamano uliooneshwa na uongozi na watu wa Sri Lanka baada ya mashambulizi.

Kupitia ukurasa wa Twitter, Mkurugenzi mkazi wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya visiwa vya bahari ya hindi, Hanaa Singer ameandika, “Umoja wa Mataifa unalaani vikali mashambulizi yaliyotekelezwa dhidi ya wananchi na waumini, rambirambi zetu kwa familia, waathirika, serikali na watu wa Sri Lanka.” Pia akawataka watu wa Sri Lanka kusimama pamoja.

Naye Rais wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Maria Fernanda Espinosa pia ameeleza kusikitishwa akiandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa yuko pamoja na watu wa Sri Lanka ambao wameathiriwa na matukio ya vurugu.

 “Tunatakiwa kuungana katika utu wetu kukemea matukio haya ya kinyama na yakome kuwalenga watu wasio na hatia, wakitekeleza imni yao kwa amani.” Amesema.

Tweet URL

 

Vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sri Lanka iliyodumu kwa miaka 26 kati ya vikosi vya serikali na makundi ya Tamil kaskazini mwa nchi, vilimalizika mnamo mwaka 2009 kwa waasi kushindwa lakini tangu wakati huo, kumekuwa na vurugu za hapa na pale na baadhi zikiwalenga makundi ya imani zenye wafuasi wachache.

Kisiwa hicho kina takribani wakristo milioni 1.5 wakatoliki lakini wakazi wengi zaidi kufikia asilimia 70 ni wa Imani ya Buddha. Pia wamo wa imani ya Hindu na waislamu wachache.

Kufuatia matukio hiyo serikali imetangaza watu kutotoka nje na pia mitandao ya kijamii inaripotiwa kufungwa.

Papa Francis kupitia hotuba yake ya Pasaka nje ya kanisa la Mtakatifu Petro mjini Roma ameeleza kusikitishwa na tukipo hilo na akaeleza kuwa yupo pamoja na waathirika wa tukio hilo la kikatili ambalo limewakuta watu wakiadhimisha sherehe muhimu ya kiimani.