Kukamatwa kwa Assange hakutositisha tathimini ya madai ya kukiukwa haki yake ya faragha:Cannataci

11 Aprili 2019

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya faragha Joe Cannataci amesema amepokea taarifa leo asubuhi za kukamatwa kwa Julian Assange mjini London Uingereza na akafafanua kwamba “hili halitozuia juhudi zangu za kutathimini madai ya bwana Assange kwamba haki yake ya faragha imekiukwa.”

Mtaalamu huyo aliyetarajiwa kukutana na Bwana Assange hivi karibuni amesema  “hii inamaanisha kwamba sasa badala ya kumtembelea na kuzungumza na Assange kwenye ubalozi wa Jamhuri ya Equador mjini London ninapanga kumtembelea na kuzungumza naye popote atakapokuwa ameshikiliwa mahabusu”

Bwana Cannataci ameongeza kuwa anaiandikia serikali ya Uingereza kuomba ruhusa ya kumtembelea Assange tarehe 25 Aprili na kuelezea hofu yake ya awali endapo atakuwa ameachiwa huru wakati huo “natumai kukutana naye akiwa mtu huru na endapo atakuwa amesafirishwa kupelekwa Marekani kama ambavyo Assange amekuwa akileza hofu yake hadharani kwamba hilo ndilo litatokea, nitaomba fursa moja kwa moja kwa serikali ya Marekani. Na popote atakapokuwa ameshikiliwa au kupelekwa wajibu wangu utamfuata.”

Amesisitiza kwamba wajibu wa mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya faragha katika kesi ya Assange utaendelea bila kuingiliwa hadi pale watakapokuwa katika nafasi ya kutoa ripoti ya tathimini yao vyovyote itakavyokuwa.

Naye mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji ya kiholela  Agness Callamard akizungumzia kukamatwa kwa Assange ameandika katika ukurasa wake wa twitter akisema kwamba “kumtimua Assange kutoka kwenye ubalozi wa Ecuador kumeruhusu Uingereza kumkamata , ikiwa ni hatua ya kwanza ya kumsafirisha kumpeleka Marekani na kumuweka katika hatari ya ukiukwaji mkubwa wa haki zake za binadamu. Uingereza imekuwa ikimshikilia bwana Assange na uwezekano wa kuhatarisha Maisha yake kwa miaka saba iliyopita.”

Julian Assange ni nani

Julian Paul Assange alizaliwa 3 Julai 1971 ni raia wa Australia ambaye ni mtaalam wa programu za kompyuta na mhariri wa Wikileaks. Hivi sasa anashikiliwa na polisi wa Uingereza kwa kukiukwa masharti ya dhamana aliyopewa 2010.

Assange alizindua Wikileaks mwaka 2006 na ilipata kufahamika zaidi kimataifa mwaka 2010 baada ya kuvujisha mlolongo wa kashfa zikiwemo za vita vya Afghanistan na vita vya Iraq. Na kufuatia kashfa hizo serikali ya Marekani ilianzisha uchunguzi wa makossa ya jinai dhidi ya WikiLeaks na kuomba msada kwa mataifa washirika.

Novemba 2010 serikali ya Sweden ilitoa kibali cha kimataifa cha kumkamata Assange ambaye miezi mitatu kabla ya hapo alihojiwa kwa madai ya ukatili wa kingono na ubakaji, madai ambayo Assange aliyakana na kusema atasafirishwa kwenda Marekani kwa sababu ya ushiriki wake katika kuchapisha nyaraka za siri za Marekani.

7 Disemba 2010 Assange alijisalimisha kwa polisi wa Uingereza lakini aliachiwa kwa dhamana baada ya siku 10 na kwa sababu ya kutofanikiwa harakati za kupinga kusafirishwa kwenda Marekani,  alikiuka masharti ya dhamana na kuamua kukimbia . Assange alipewa hifadhi na Ecuador mwezi Agosti 2012 na akasalia kwenye ubalozi wa Ecuador Uingereza mpaka leo Aprili 11, mwaka 2019 alipokamatwa. Na Assange amekuwa na uraia wa Ecuador tangu 12 Disemba 2017.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter