Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Australia tafadhali wapeni huduma ya afya wakimbizi na wanaoomba hifadhi-Wataalamu wa UN

Mwaka 2014 Australia ilikuwa na mpango wa kuwahamisha wakimbizi kutoka kambi hii iliyoko katika kisiwa cha Nauru kwenda Cambodia
UNHCR/N. Wright
Mwaka 2014 Australia ilikuwa na mpango wa kuwahamisha wakimbizi kutoka kambi hii iliyoko katika kisiwa cha Nauru kwenda Cambodia

Australia tafadhali wapeni huduma ya afya wakimbizi na wanaoomba hifadhi-Wataalamu wa UN

Haki za binadamu

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, hii leo mjini Geneva Uswisi wameisihi Australia kuwapatia kwa haraka huduma ya afya wasaka hifadhi zaidi ya 800 na wahamiaji wengine ambao wamekuwa wakishikiliwa katika kambi zilizoko katika fukwe za nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano bila suluhisho. 

Wataalamu hao huru wametoa wito kwa serikali ya Australia kuwahamisha wale ambao wametambuliwa kuwa wanahitaji huduma za haraka za matibabu.

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wana wasiwasi mkubwa kuwa hali ya watu hao imekuwa ikizorota na kusababisha matukio mabaya ambapo kumekuwepo na ripoti kadhaa watu kujiumiza na pia majaribio ya kujiua.

Wataalamu wamekuwa wakiwasiliana na serikali ya Australia ambapo barua ya mwisho iliyoandikwa kwa serikali ikieleza hali hiyo, ilitumwa Aprili pili mwaka huu wa 2019 ambapo serikali ilijibu mnamo tarehe 3 mwezi huu wa Juni 2019.

Wataalamu wanasema, “Australia inatakiwa kuangalia masuluhisho ya muda mrefu kwa ajili ya wahamiaji wakati suluhisho haliwezi kupatikana katika kambi zilizoko ufukweni.”

Katika majibu yake, serikali ya Australia imesema, “hakuna ambaye amenyimwa huduma ya afya.” Hata hivyo taarifa zilizopokelewa tangu mwaka 2014 zinaeleza kuwa visa kadhaa vya vifo viliripotiwa kutokana na ukosefu wa huduma za afya ikiwemo matibabu katika kambi hizo.

Wataalamu hao wa haki za binadamu wamesema wanasikitika kuwa baadhi ya kambi walimowekwa wahamiaji na wasaka hifadhi zinafanana na vifungo na hazifai kutumika kuwapokea wasaka hifadhi na wakimbizi.