Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapato ya fedha yasihatarishe maisha ya abiria na wafanyakazi wa ndege za kiraia- Mtaalamu

Agnès Callamard, Mtaalamu maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa
UN /Manuel Elias
Agnès Callamard, Mtaalamu maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa

Mapato ya fedha yasihatarishe maisha ya abiria na wafanyakazi wa ndege za kiraia- Mtaalamu

Haki za binadamu

Mtaalamu maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Agnès Callamard  amesema kanuni za ulinzi wa ndege za kiraia zinazoruka kwenye maeneo ya mizozo ya kijeshi zisiwe na utata wowote na ziwe wazi ili kulinda maisha ya abira na wafanyakazi wa ndege hizo.
 

Amesema hayo leo kupitia taarifa yake iliyotolewa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, mjini Geneva, Uswisi, ikiwa ni kuelekea mwaka mmoja tangu ndege ya kiraia ya Ukraine, PS752 itunguliwe na kuua watu wote 176 waliokuwemo ndani yake.

Ndege hiyo ilitunguliwa tarehe 8 mwezi Januari mwaka 2020 wakati ikiwa safarini kutoka Tehran, Iran kuelekea Kiev nchini Ukraine, na ilitunguliwa kwa makombora mawili kutoka Iran, katika tukio ambalo lilielezwa lilifanyika wakati kuna mvutano mkubwa kati ya Iran na Marekani.

Bi. Callamard amesema, “kutunguliwa kwa ndege hiyo kunaangazia kasoro katika mikataba ya kimataifa kuhusu usafiri wa safari za anga, katika kuzuia mivutano ya kijeshi dhidi ya ndege za kiraia na katika kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika”.

Amesema tukio hlo ambalo lingaliweza kuzuilika, sasa linahitaji hatua za dharura kutoka kwa wadau wote ikiwemo serikali na mashirika ya ndege.

Nchi na mashirika ya ndege waache tamaa

Katika kuepusha tukio kama hilo siku za usoni na kuhakikisha ulinzi wa abiria kwenye ndege za kiraia zinazoruka maeneo yenye mizozo ya kijeshi, Bi. Callamard ametoa mapendekezo ikiwemo, “katika maeneo yenye mivutano ya kijeshi, yawe yanatambulika kuwa ni mizozo ya kivita au la, njia ya msingi zaidi ya kuzuia mashambulizi dhidi ya ndege za kiraia ni kufunga anga la eneo husika. Hatua nyingine zozote ziwe za nyongeza. Hata hivyo mara nyingi seriklai zinashindwa kufanya hivyo kwa sababu za kibiashara au kisiasa.”

Halikadhalika amesema jamii ya kimataifa lazima iweke kanuni za wazi na zisizo na utata kuhusu ni wakati gani nchi inapaswa kufunga anga lililo chini ya mamlaka yake, na iwapo nchi itashindwa kufanya hivyo, au hata kudhibiti upitaji wa ndege, basi  nchi hiyo ichukue hatua za haraka kuzuia ndege zisipite maeneo yenye mzozo.

Halikadhalika ametoa wito kwa mashirika ya ndege kupatia umma ramani za safari zao za ndege na yaimarishe uwezo wao wa kutathmini hatari ikiwemo kuzingatia kanuni za juu kabisa za kupata taarifa kuhusu usalama wa njia ambamo ndege hiyo itapita.

Amesisitiza kuwa abiria na wafanyakazi wa kwenye ndege hawapaswi kuweka rehani na mashirika na nchi ambazo zinapatia kipaumbele faida na mapato badala ya usalama wa abiria na wafanyakazi.

Tayari mtaalamu huyo maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameandika barua serikali ya Iran kuhusu kutunguliwa kwa ndege hiyo ya Ukraine.
TAGS: Ukraine,  Agnès Callamard