Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana tunyanyuane hii itatusaidia zaidi- Jayathma

Rais wa ECOSOC, Inga Rhonda King (Katikati) akihutubia jukwaa la vijana la baraza hilo la uchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa.
UN / Evan Schneider
Rais wa ECOSOC, Inga Rhonda King (Katikati) akihutubia jukwaa la vijana la baraza hilo la uchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa.

Vijana tunyanyuane hii itatusaidia zaidi- Jayathma

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Jukwaa la vijana la Baraza la Uchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC, limeanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani likileta pamoja wawakilishi zaidi ya 1000 wa vijana kutoka kona mbalimbali pamoja na mawaziri wa vijana kutoka nchi wanachama wa umoja huo kuzungumzia harakati za kunasua vijana na kile kinachofanyika mashinani kuchagiza mchango wa vijana katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Miongoni mwa washiriki ni mwanaharakati wa vijana Virbu Sharma ambaye yeye ameangazia zaidi utekelezaji wa lengo namba 4 la maendeleo endelevu kuhusu elimu na elimu jumuishi akimulika mkakati wa Umoja wa Mataifa uitwao Generation Unlimited unaolenga kufanya kazi na vijana na kwa ajili ya vijana.

Mkakati huo ambao Virbu ni mjumbe wa bodi, umejikita katika elimu ya sekondari, kuendeleza stadi na uwezeshaji wa vijana walio hatarini ikiwemo wale wenye ulemavu.

“Mathalani nchini Paraguay, walimu 1000 walifundishwa na kupatiwa ujuzi wa jinsi ya kuanzisha elimu jumuishi.”

Amesema yeye kwa upande wake licha ya kuwa mshauri kwa watoto  wenye ulemavu, anahusika pia na jukumu la kutafiti kubaini mifano bora zaidi ya elimu jumuishi na vifaa vya usaidizi kwa ajili ya watoto wenye ulemavu.

Kauli pia zilisikika kuhusu kile ambacho vijana wanafanya katika kusongesha lengo namba 16 la amani, haki na taasisi thabiti ambapo Liberia ilimulikwa kwa kuzingatiwa kuwa asilimia 63 ya wananchi wake ni vijana wenye umri wa chini ya miaka 25.

Waziri wa vijana na michezo nchini Liberia Dester Zeogar Wilson aliulizwa ni dhima gani ambavyo vijana walichangia kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika  mwaka 2017 ambapo amesema kabla ya uchaguzi vijana kutoka vyama vya siasa vilivyopo kwenye kaunti 10 kati ya 15 walishiriki kwenye mashauriano ya amani .

Ndani  ya ukumbi wa wa Baraza la Wadhamini la Umoja wa Mataifa, ambako kumefanyika mkutano wa jukwaa la vijana.
UN / Evan Schneider
Ndani ya ukumbi wa wa Baraza la Wadhamini la Umoja wa Mataifa, ambako kumefanyika mkutano wa jukwaa la vijana.

Amesema vijana hao walielimishwa kuhusu umuhimu wa utawala bora wa kidemokrasia kwenye jamii, na usimamizi wa chaguzi pamoja na kuepusha mizozo.

“ Mashauriano haya yalikuwa na maana sana. Vijana hao walikuwa mabingwa  wa kueneza mchakato wa upigaji kura usio na ghasia. Walisambaza vikaragosi mnato, vipeperushi na mabango kwenye jamii zao yenye ujumbe wa kuchaguzi  mchakato wa amani wa uchaguzi.”

Mapema akifungua mkutaon huo Rais wa Baraza la Uchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC, Inga Rhonda King amesema changamoto za sasa hazitambua mipaka akitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi au hata uhamiaji.

“Changamoto hizi zinahitaji suluhu za kimataifa ambazo zinaweza kupatikana kupitia maafikiano ya kimataifa. Umoja wa Mataifa uko hapa kuhudumia dunia na kuwahudumia ninyi,” amesema Bi. Inga mbele ya wajumbe hao wakijumuisha mawaziri 34.

Tweet URL

Kwa upande wake mjumbe wa maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Vijana, Jayathma Wickramanayake amewakumbusha vijana kuwa waendelee kujiamini na kuchanua lakini la msingi “msisahau kuwanyanyua wale walio kama ninyi kwasababu kwa pamoja tunaweza kuwezesha, kujumuishana na kuwa sawa.”

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa naye alipozungumza na vijana na washiriki wa jukwaa hilo ametaja maeneo matatu ambayo ni muhimu kuwa ushirikiano wa dhati kati ya kizazi na kizazi, ajira kwa vijana zaidi na ushiriki wa vijana kwenye amani na usalama.

Mkutano huu wa siku mbili unatathmini malengo endelevu, namba 4 la elimu jumuishi, namba 8 la ukuaji jumuishi, namba 10 kuhusu ukosefu wa usawa, namba 13 la hatua kwa mabadiliko ya tabianchi, namba 16 kuhusu jamii zenye amani na taasisi thabiti pamoja na namba 17 linaloangazia mbinu za kufanikisha malengo hayo yote ambayo ni muhimu kwa vijana.