Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Naondoka Libya na moyo mzito- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alipokuwa ziarani kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli. (Aprili 2019)
UN/Mohammed Omar Omar
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alipokuwa ziarani kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli. (Aprili 2019)

Naondoka Libya na moyo mzito- Guterres

Amani na Usalama

Naondoka Libya nikiwa na hofu kubwa na moyo mzito. Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyotoa leo wakati akizungumza na waandishi wa habari huko Benghazi nchini Libya kabla ya kuondoka nchini humo.

Bwana Guterres ambaye alikuwepo ziarani Libya jana akiwa Tripoli, leo alikuwa mjini Benghazi ambako amekutana na Haftar, Kamanda wa jeshi la kitaifa la Libya kwa lengo la kupatia msisitizo hoja yake ya kuwa amani ya Libya inapatikana kwa njia ya mazungumzo na si vinginevyo.

Katibu Mkuu amewaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo kuwa bado anaamini kuna uwezekano wa kuepusha umwagaji damu na mizozo kwenye mji mkuu Tripoli na viunga vyake.

Hata hivyo amesema, “Umoja wa Mataifa unasalia tayari kufanikisha suluhu yoyote ya kisiasa yenye lengo la kuungainsha taasisi za Libya. Chochote kitakachotokea, Umoja wa Mataifa bado umejizatiti kusaidia wananchi wa Libya. Walibya wana haki ya kupata amani, usalama, ustawi na haki zao za binadamu ziheshimiwe.”

Hapo jana akiwa Tripoli, Katibu Mkuu alisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa hauna ajenda binafsi wala maslahi kuhusu Libya isipokuwa ustawi wa watu wa Libya, amani na uwezekano wa kuishi katika demokrasia ya kawaida na wananchi kufaidika na utajiri mkubwa wa nchi.

Baada ya ziara yake Libya, Katibu Mkuu hivi sasa yuko njiani kuelekea nchini   Jordan ambapo kesho atahutubia mkutano wa jukwaa la kiuchumi duniani na atarejea New York, Marekani siku ya  Jumapili.