Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Agenda pekee ya UN nchini Libya ni 'Ustawi wa watu wa Libya'-Antonio Guterres.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akikutana na wakimbizi na wahamaiaji katika kituo mjini Tripoli, Libya. 4 April 2019.
UN Spokesperson/Florencia Soto Niño
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akikutana na wakimbizi na wahamaiaji katika kituo mjini Tripoli, Libya. 4 April 2019.

Agenda pekee ya UN nchini Libya ni 'Ustawi wa watu wa Libya'-Antonio Guterres.

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa ziarani nchini Libya, amewaambia wanahabari hii leo mjini Tripoli kuwa watu wa Libya wamepata shida nyingi na sasa wanastahili kuishi katika nchi ya kawaida wakiwa na taasisi za kawaida za kisiasa, wakiwa na amani na usalama pamoja na ustawi.

Aidha Bwana Guterres amefafanua kuwa Umoja wa Mataifa hauna ajenda binafsi wala maslahi kuhusu Libya isipokuwa ustawi wa watu wa Libya, amani na uwezekano wa kuishi katika demokrasia ya kawaida na wananchi kufaidika na utajiri mkubwa wa nchi.

 “Na ndiyo sababu tunaamini kwamba suluhisho la kisiasa kwa Libya linahitaji kuwa suluhisho la kisiasa lililoongozwa na walibya wenyewe na kwa ajili ya walibya. Si kwa njia ya uingiliaji wa kigeni kwamba tutaweza kutatua matatizo ya nchi yoyote na hivyo ni muhimu kwamba kanuni hiyo inatumika pia kwa Libya.” Amesema Bwana Guterres.

Katibu Mkuu amesema kutokana na hali hiyo ndiyo maana Umoja wa Mataifa kwa mashauriano na walibya kote nchini walikubaliana kuwa kuwe na mkutano wa kitaifa wa walibya ambao utaamua mstakabali wa Libya ikiwemo kuelekea uchaguzi. Mkutano huo unategemewa kufanyika katika mji wa Ghadames nchini Libya mwezi huu wa April tarehe 14 hadi 16.

Mkutano huo unategemewa kufungua njia ya kukomesha kipindi cha mpito cha miaka 8 kwa kuunganisha taasisi za nchi na kutengeneza njia ikiwa ni pamoja na kupata tarehe kwa ajili ya uchaguzi utakaowashirikisha wote na ukiwa wa huru na haki.

Hakuna suluhisho la kijeshi

Aidha Bwana Guterres amesisitiza kuwa njia ya mazungumzo ni nzuri zaidi kufikia muafaka kuliko kutumia nguvu za kijeshi, “nilipokuwa ninakuja hapa Libya nimeshangazwa na idadi ya wanajeshi na kwa hivyo imenitia wasiwasi. Ninataka kutoa ombi kwa majeshi yote kusitisha harakati na naomba utulivu. Na katika mkutano niliokuwa nao na rais wa baraza tumetambua kuwa hakuna suluhisho la kijeshi kwa tatizo lolote duniani na hakuna ufumbuzi kwa matatizo nchini Libya. Suluhisho linatakiwa kuwa la kisiasa n ani muhimu kwamba suluhisho la kisiasa ni la nguvu sana hasa kupitia katika mazungumzo. Na ni naamini ni muhimu kuanza tena majadiliano na mimi mwenyewe kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Niko tayari kuchukua hatua ambayo inaweza kuwa muhimu kwa hilo kuwezekana.”

Tweet URL

 

Vile vile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametembelea kituo ambako wakimbizi na wahamiaji wanazuiliwa na anasema amesitikitishwa na kushitushwa na kiwango cha mateso na pia hali ya kukata tamaa aliyoikuta.

“Hili bila shaka si jukumu la Libya pekee bali ni la jumuiya nzima ya kimataifa.”

Bwana Guterres Ijumaa hii anategemewa kufika mjini Benghazi kukutana na Haftar, Kamanda wa jeshi la kitaifa la Libya. Na alipoulizwa na wanahabri ni kitu gani anakusudia kuzungumza na kamanda huyo Bwana Guterres amesema asingependa kamanda huyo apate taarifa za mkutano wao kupitia vyombo vya habari lakini muhimu ni kutambua kama alivyosema awali, amani ya Libya itapatikana kwa njia ya mazungumzo na si vinginevyo.