Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi waongezeka Chad, ukata watia shaka operesheni za usaidizi

Kambi ya Gubio Maiduguri imepokea wakimbizi wapya 4500 tangu Novemba 2018, wengi wao katika wiki za karibuni kufuatia mashambulizi ya kundi lenye silaha la Baga, karibu na ufukwe wa ziwa Chad, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria
OCHA/Leni Kinzili
Kambi ya Gubio Maiduguri imepokea wakimbizi wapya 4500 tangu Novemba 2018, wengi wao katika wiki za karibuni kufuatia mashambulizi ya kundi lenye silaha la Baga, karibu na ufukwe wa ziwa Chad, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria

Wakimbizi waongezeka Chad, ukata watia shaka operesheni za usaidizi

Msaada wa Kibinadamu

Ghasia za mwezi uliopita kwenye jimbo la Diffa lililopo mpakani mwa Niger na nchi za Nigeria na Chad zimesababisha ongezeko la wakimbizi wa wa ndani na vifo vya raia 88.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na usaidizi wa dharura, OCHA imesema ghasia hizo zinatokana na mashambulizi yapatayo 21 dhidi ya raia na wanajeshi kuwa kwenye jimbo hilo lililopo kusini-mashariki mwa Niger.

Msemaji wa OCHA mjini Geneva, Uswisi, Jens Laerke amewaambia waandishi wa habari kuwa mashambulizi hayo yanafanywa na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram kwenye bonde la Ziwa Chad.

Amesema idadi hiyo ya vifo 88 kwa mwezi mmoja pekee uliopita ni kubwa ikilinganishwa na jumla ya vifo 107 vilivyoripotiwa mwaka mzima wa 2018 na kwamba OCHA nchini Niger ina hofu k ubwa kuhusu kubadilika kwa  mwelekeo wa ghasia  unaotia mashakani mustakabali wa raia.

Bwana Laerke amesema mashambulio hayo 21 yamesababisha watu wapatao 18,500 kukimbilia eneo la mjini huko Diffa na kwingineko ambako tayari kuna hifadhi wakimbizi wa ndani 100,000 na wakimbizi 120,000.

Akifafanua mgawanyiko wa wakimbizi hao wa ndani Bwana Laerke amesema ,“maeneo yanayohifadhi watu wengi zaidi ni Awaridi ambako kuna wakimbizi wa ndani 8,000 kwenye wilaya ya mjini ya Diffa, huko Kindjandi watu 2,500 kwenye kitongoji cha Gueskérou. Timu ya usaidizi wa kibinadamu nchini humo  itaendelea na operesheni zake kwenye maeneo hayo licha ya ongezeko la ghasia na tathmini tano za haraka zimefanyika ambapo matokeo ya awali yanaonyesha kuwa watu wanahitaji maji, huduma za kujisafi, makazi, chakula na vifaa vya nyumbani.”

OCHA inasema wakati idadi ya wahitaji inaongezeka, rasilimali nazo ni adimu ambapo fedha za dharura zilizotolewa ni kidogo wakati huu ambapo katika ombi la dola miliolni 383 za kusaidia Niger mwaka huu wa 2019, ni asilimia 3 tu zimepatikana.