Msaada wa kibinadamu wahitajika Niger, watoto taabani

2 Julai 2021

Zaidi ya watu Milioni 3.8 wakiwemo watoto Milioni 2.1, wanahitaji msaada wa kibinadamu nchini Niger, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. 

Kaimu Mwakilishi wa UNICEF nchini humo, Aboubacry Tall amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo kuwa idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na mwaka jana 2020 na chanzo ni migogoro isiyoisha, kuhamahama, ukosefu wa chakula, Utapiamlo, magonjwa ya mara kwa mara ya mlipuko, mafuriko na ukame.

Bwana Tall amesema idadi kubwa ya watu hao wako maeneo ya ndani ambayo watoa huduma za kibinadamu hawawezi kuyafikia kwa urahisi.

“Maeneo yasiyo salama ni mengi na yanazidi kuongezeka nchini Niger. Mashambulizi karibu na mipaka na Burkina Faso, Mali na Nigeria yanasababisha ongezeko la wakimbizi nchini humo na hali za kimaisha za mamia ya maelfu ya watoto zinazidi kudorora,” amesema Bwana Tall.

Mathalani amesema mashambulizi mpakani mwa Niger na Burkina Faso na Mali yameongeza mahitaji ya kibinadamu huko Tillabéry na Tahoua, ambako kuna zaidi ya wakimbizi 195,000.
Mashambulizi dhidi ya raia katika eneo la Ziwa Chad yamezuia watu zaidi ya 269,000 washindwe kurejea nyumbani.

Hata hivyo Kaimu Mwakilishi huyo amesema pamoja na ukosefu wa rasilimali, wenyeji wameendelea kukarimu wakimbizi na kugawana hata kile kidogo walicho nacho.
“Watoa misaada ya kibinadamu ni jamii yenyewe. Wanaleta chakula, malazi, huduma za afya na ulinzi pamoja na matumaini kwa wale walio kwenye shida. Huu ni mfano halisi ambao raia wa Niger wanaonesha ulimwenguni,” amefafanua Bwana Tall.

Sambamba na ukosefu wa usalama, vikwazo vilivyowekwa na serikali vya watu kutembea vinakwamisha pia huduma za kibinadamu kwenye maeneo yenye mzozo na hivyo UNICEF inatoa wito kwa pande zote zinazokinzana kuheshimu kanuni za kibinadamu za kutoa fursa ya kusambaza misaada kwa amani na usalama.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter