Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu wakimbilia Chad kufuatia kuibuka kwa mapigano mapya nchini Nigeria.

Watoto kutoka katika familia zilizoparaganyika katika eneo la Maiduguri, jimboni Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria wakikinga maji. Mgogoro katika eneo hilo umewalazimisha mamia ya maelfu kuyahama makazi yao na kuishi kwa kutegemea misaada.
UNICEF/Gilbertson VII Photo
Watoto kutoka katika familia zilizoparaganyika katika eneo la Maiduguri, jimboni Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria wakikinga maji. Mgogoro katika eneo hilo umewalazimisha mamia ya maelfu kuyahama makazi yao na kuishi kwa kutegemea misaada.

Maelfu wakimbilia Chad kufuatia kuibuka kwa mapigano mapya nchini Nigeria.

Wahamiaji na Wakimbizi

Kuongezeka  kwa vurugu mpya kaskazini mashariki mwa Nigeria kumewalazimisha maelfu ya watu, wengi wao wakiwa  wanawake na watoto kukimbilia nchini Chad. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linakadiriwa kuwa wakimbizi 6,000 wamekimbia jimbo la Borno kuanzia tarehe 26 mwezi uliopita, baada ya mapigano kuanza kati ya vikosi vya serikali na makundi yenye  silaha katika mji wa Baga karibu na mpaka wa Chad.

Yaelezwa kuwa wakimbizi wengi walivuka ziwa Chad na kufika katika Kijiji cha Ngouboua kilichoko katika fukwe za ziwa Chad kilomita 20 kutoka mpaka wa Nigeria. Inachukua saa tatu kuvuka mto huo na wamesema wanakimbia baada ya vitisho vya ulipizaji visasi na manyanyaso kufuatia mashambulishi ya kijeshi.

Msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi, Charles Yaxley akizungumza na waandishi wa habari hii leo amesema kinachofanyika hivi sasa..

“UNHCR na mamlaka za Chad wanawaandikisha na kuwakagua wakimbizi wapya wanaofika ili kutathimini kiwango cha mahitaji kwa ajili ya usaidizi. Wengi wa wanaoingia kwa mujibu wa tathimini ya UNCHR ni wanawake na Watoto ambao ni asilimia 55.”

Halikadhalika amesema..

"Tuko mbio kuhakikisha tunatoa kwa wakati malazi na misaada mingine kwa wale wanaofika ikiwemo wale walioko katika hatari zaidi. Kwa sasa waliofika wako katika makazi ya pamoja. UNHCR inasambaza vifaa vya kuwapa unafuu kama blanketi, magodoro na vyandarua, pia wakimbizi wanapata chakula cha moto”

Juhudi za UNHCR zinaendelea kuwahamisha wakimbimbizi kutoka katika fukwe za ziwa Chad kutokana na sababu za kiusalama na baada ya serikali kuomba hivyo. Hadi sasa UNHCR inasema imewahamisha wakimbizi wapatao 4,200 kwenda katika kambi ya Dar es Salam ambayo iko kilomita 45 kutoka ufukweni. Kambi hiyo tayari ina wakimbizi kutoka Nigeria wapatao 11,300 ambao walifika mwaka 2014.

Ndani ya Nigeria mapigano hayo yamewalazimisha maelfu ya raia kuyakimbia makazi yao zaidi ya watu 30,000 wakifika Maiduguri idadi kubwa zaidi kuzidi uwezo wa kambi zilizopo ambazo tayari zinawahifadhi wakimbizi wa ndani.

UNHCR imesema pia inafuatilia mstakabali wa wakimbizi wa Nigeria wapatao 9,000 ambao iliripotiwa kuwa walifurushwa kutoka Cameroon wiki iliyopita. UNHCR imeziomba nchi kuiacha mipaka yao wazi ili kuwapokea wakimbizi wanaoyakimbia mapigano nchini Nigeria.