Licha ya mafanikio operesheni za ulinzi wa amani zinakabiliwa na changamoto kubwa:Guterres

29 Machi 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema licha ya hatua kubwa na mafanikio yaliyopatikana kwenye operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa bado kuna pengo kubwa hasa la vifaa , fedha na miundombinu mingine ya msingi na kuzitaka nchi na wafadhili kunyoosha mkono zaidi kusaidia.

Guterres ameyasema hayo leo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa operesheni za ulinzi wa amani ngazi ya mawaziri kwenye Baraza kuu la Umoja huo mjini New York Marekani na kuongeza kuwa“Kwa miongo mingi operesheni zetu za ulinzi wa amani zimesaidia nchi nyingu kuanzia Liberia na Sierra Leon hadi Timor Leste na Cambodia kutoka kwenye machafuko na kuingia kwenye amani . Wanalinda maelfu ya raia , kusaidia suluhu za kisiasa katika migogoro na kusaidia kulinda usitishaji wa mapigano.”

Ameongeza kuwa lakini migogoro ikiendelea kuongezeka kuwa migumu na ya hatari zaidi operesheni za Umoja wa Mataifa lazima ziongeze kasi pia kwani maisha ya walinda amani wengi yanapotea akitolea mfano mwaka 2018 ambapo walinda amani 27 waliuawa kwenye machafuko.

Amesisitiza kuwa kipaumbele cha Umoja wa Mataifa ni kufanya operesheni hizo za ulinzi wa amani kuwa salama na imara ambao pia ni makakati wake ukiujumisha kuelekeza nguvu kwenye matarajio yanayowezekana na kuchagiza msaada kwa ajili ya suluhu za kisiasa kwenye migogoro.

Amesema tayari kunashuhudiwa matokeo chanya kwa mfano kupungua sana kwa idadi ya walinda amani wanaouawa kwenye operesheni mbalimbali akitaja kama vile Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR. Hata hivyo ameonya kwamba“Lakini bado tunapungukiwa uwezo muhimu kama ambavyo azimio la kushirikiana majukumu lilivyoweka bayana, ni lazima tuzibe pengo hili kwa pamoja.”

Akitoa mfano Guterres amesema kunahitajika haraka magari ya kubebea askari na silaha ambayo yataimarisha fursa za kunusirika na mashambulizi . Zaidi ya walinda amani 119 wameuawa Mali na 397 kujeruhiwa nchini humo tangu kuanzisha kwa mpango wa Umoja wa Mastaifa Mali MINUSMA  mwaka 2013. 

Amesema CAR nayo inahitaji msaada wa helkopta ambazo zinaweza kufanya kazi saa 24 kwa ajili ya kutoa msaada wa kitabibu na kusafirisha majeruhi kutoka maeneo ya vijijini. Kwengineko amesema msaada wa kijasusi unahitajika, uchunguzi, kikosi cha dharura na timu ya anga ya madaktari wa dharura wa kuwahamisha majeruhi.

Kuhusu kuongeza idadi a walinda amani wanawake amesema idadi imeongezeka Karibu mara mbili ya maafisa wanawake na waangazili tangu mkutano wa Vancouver na wengi wanapelekwa katika operesheni mchanganyiko za polisi na wanajeshi na ameipongeza serikali ya Canada kwa kuanzisha mradi wa Elsie kwa ajili ya wanawake katika operesheni za ulinzi wa amani. Hata hivyo amesema“Lakini tunahitaji kuongeza juhudi zaidikwa sababu haikubaliki kwamba kwa mwaka 2019 ni asilimia 4 tu ya walinda amani wetu ni wanawake. Tutawasilisha mkakati wa kuongeza idadi ya walindamanai wanawake kwenye Baraza la Usalama mwezi ujao na ninaomba msaada wenu.”

Amemalizia kwa kusema upungufu wa fedha unaozikabili operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa ni changamoto kubwa ambayo ametoa wito kwa nchi wanachama kusaidia kuitatua akisema ili kusongesha mbele ajenda ya kulinda raia na kuleta amani ya kudumu ushirika imara wa kimataifa ndio suluhu.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter