Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suluhu za kisiasa ni kiungo muhimu cha amani ya kudumu- Lacroix

Mjini Beni, DRC walinda amani kutoka Malawi wakizingira kijiji kabla ya kushika doaria.
UN News/Joon Park
Mjini Beni, DRC walinda amani kutoka Malawi wakizingira kijiji kabla ya kushika doaria.

Suluhu za kisiasa ni kiungo muhimu cha amani ya kudumu- Lacroix

Amani na Usalama

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa, Jean-Pierre Lacroix amesisitiza kwamba ulinzi wa amani unasalia kuwa nguzo ya mataifa mengi isiyokwepeka kwa ajili ya kuzuia mizozo na kupunguza hatari ya kutofikia amani ya kudumu.

Akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo bwana Lacroix amesema ,walinda amani wa Umoja wa Mataifa wana mchango mkubwa katika kuzuia migogoro wanapopelekwa na kulinda mamilioni ya watu walio hatarini kote ulimwenguni.

Hii imekuja mwaka mmoja na nusu tangu kuzinduliwa kwa kampeni ya hatua za pamoja kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa amani A4P huku bwana Lacroix akimulika hatua zilizopigwa na yanayosalia.

Mkuu huyo amesema suluhu za kisiasa ni kiungo muhimu kwa ajili ya amani ya kiudumu ambayo ipo kwenye kiini cha ajenda ya A4P. Ameongeza kwamba, “katika kila nchi pale ambapo tunatumwa na ndani ya uwezo wa mamla, ujumbe wetu huzingatia na huwacha nafasi ya kusaka suluhu za kisiasa.” Akitolea mfano ujumbe wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, Darfur na Mali.

Bwana Lacroix amesema, “kuimarika kwa uelewa wa hali ni kiungo kingine  muhimu kwa ajili ya operesheni zenye kuzaa matunda, na tunapiga hatu katika hilo.”

Ameongeza kwamba mifumo ya kuratibu na kufuatilia intelijensia ya ujumbe wa ulinzi wa amani umeanzishwa katika operesheni za ulinzi wa amani Mali, DRC, CAR na Sudan Kusini, “kwa jili ya kuhakikisha uratibu kati ya wadau wote husika wa intelejensia ya ulinzi wa amani chini ya uongozi wa mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu.

Mkuu huyo wa operesheni za ulinzi wa amani amesema mbinu hizo tayari zinaimarisha utendaji na utaratibu kati ya jeshi, polisi na raia.

Kuhusu tuhuma za  ukatili wa kingono na unyanyasaji SEA, zinazotekelezwa na walinda amani, bwana Lacroix amesema, “tumeona kupungua kwa tuhuma za vitendo hivyo kutoka vtuhuma 104 mwaka 2016 hadi 55 mwaka 2018,” ameongeza kwamba, “iwapo tutafikia lengo ya kuimraisha vita dhidi ya SEA katika ulinzi wa amani, tunahitaji ushiriki kikamilifu kutoka kwa vikosi vyote na polisi kutoka nchi wachangiaji vikosi.

Kufikia Julai 12 mwaka huu wa 2019, nchi 152 zimeridhia tamko la A4P na dhamira za pamoja.