Kongamano la UN lafungua pazia wito ukitolewa wa ujumuishaji na usawa Asia Pacific

27 Machi 2019

Mwaka huu wa 2019 utakuwa ni muhimu katika kufikia ajenda ya maendeleo ya mwaka 2030 na majukwaa kutoka mabara yote yatatengeza njia kuweza kujitathmini katika hatua zilizopigwa kuelekea kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed katika hotuba yake ya jukwaa la sita la Asia Pacific kuhusu malengo endelevu (APFSD) lililofungua pazia leo Jumatano mjini Bangkok, Thailand huku wito ukitolewa kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha uwezeshaji, ujumuishwaji na usawa kwa ajili ya kufikia ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu au SDG’s.

Licha ya hatua zilizopigwa kiuchumi na kiteknolojia makadirio ya sasa yanaonyesha kwamba ufikiaji wa malengo 17 SDGs katika ukomo wake 2030 hautawezekana ingawa bi Mohammed amesimu juhudi za eneo hilo

( Amina J. Mohammed)

Katika kipindi cha miaka michache, nimetizama na kutiwa moyo na hatua zilizopigwa na mataifa ya Asia na Pacific katika juhudi za kuelekea malengo ya maendeleo  endelevu. Serikali zenu zimechukua changamoto ya ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu kwa uongozi thabiti. Mmepiga hatua katika kuimarisha takwimu, ushirikiano katika kuimarisha sera zinazozingatia binadamu, mipango na programu.

Washiriki katika jukwaa la sita kuhusu malengo ya maendeleo endelevu mjini Bangkok Thailand (APFSD) lililoandaliwa na Umoja wa Mataifa ESCAP
ESCAP Photo
Washiriki katika jukwaa la sita kuhusu malengo ya maendeleo endelevu mjini Bangkok Thailand (APFSD) lililoandaliwa na Umoja wa Mataifa ESCAP

Hata hivyo ametoa angalizo

( Amina J. Mohammed)

“Katika ukanda wa Asia Pacific, ongezeko la ukosefu wa usawa ni kizuizi kikubwa katika kuongeza maendeleo. Ukosefu wa usawa katika mali, ufikiaji wa huduma za msingi na ukosefu wa usawa wa uwezo wa kuibuka kutoka kwenye changamoto na kushughulikia madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi vyote vimeongezeka.”

Kwa mantiki hiyo naibu katibu mkuu ametoa pendekezo la kubadili hali hiyo, mosi ni kuvunja minyororo inayokwamisha utekelezaji wa sera katika misingi ya sekta muhimu akisema kwamba kunapaswa kuwa na hali ya kuondoka kutoka malengo ya maendeleo ya millenia hadi SDGs, pili nia zinapaswa kuendana na uwekezaji na kujumuisha sekta zote katika kufikia malengo ya pamoja.Tatu ni kuimarisha ushirikiano kwa viwango vya juu. 

Kwa upande wake mwakilishi wa katibu mkuu na katibu mkuu wa kamisheni ya uchumi na jamii kwa ukanda wa Asia na Pacific (ESCAP) Armida Alisjahbana akihutubia kongamano hilo amesisitiza umuhimi wa uwekezaji katika sekta muhimu za kijamii.

“Ili kufikia ajenda ya 2020, kuongeza uwekezaji kunahitajika ili kuimarisha kasi ya hatua. Tathmini ya awali inaonyesha kwamba nchi nyingi zina uwezo wa kifedha, licha ya kwamba maeneo ambako fedha zinahitajika inatofautiana kutoa eneo na linguine kwa mujibu wa ukubwa na utofauti wa Asia na Pasifiki. Kile ambacho ni dhahiri ni kwamba kuwawezesha watu na kuhakikisha ujumuishwaji na usawa-kauli mbiu ya kongamano hili vinaweza kuchochea hatua kuelekea malengo yote ya SDGs.”

Kongamano hilo la kila mwaka ambalo huleta watu pamoja kutoka serikalini, maafisa wa Umoja wa mataifa na sekta binafsi na vyama vya kiraia katika kipindi cha siku tatu litatathmini hatua zilizopigwa katika malengo ya maendeleo endelevu ikiwemo SDG4 la elimu bora, SDG8 la ajira bora na elimu, SDG10 la kupunguza ukosefu wa usawa, SDG13 ya hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, SDG 16 la amani, haki na taasisi dhabiti na SDG17 la ushirikiano kwa ajili ya malengo.

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter