Italia imekiuka haki kumshurutisha mwanamke kubeba ujauzito kisha ukatoka:UN

Ukumbi wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambamo kwalo wataalamu wa haki za binadamu huchangia hoja kuhusu haki za binadamu
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Ukumbi wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambamo kwalo wataalamu wa haki za binadamu huchangia hoja kuhusu haki za binadamu

Italia imekiuka haki kumshurutisha mwanamke kubeba ujauzito kisha ukatoka:UN

Haki za binadamu

Uamuzi uliotolewa leo na kamati ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kiuchumi, kijamii na haki za kitamaduni umesema Italia ilikiuka haki za binadamu za kiafya za mwanamke mmoja baada ya sheria za masuala ya tiba ya uzazi nchini humo kumlazimisha kubeba ujauzito ambao hatimaye ulitoka.

Maamuzi hayo yaliyotolewa mjini Geneva Uswis na jopo la watu 18 wataalam huru wa kimataifa wa kati ya haki za binadamu yamefikiwa baada ya waathirika mwanamke na mwanaume kwa pamoja kuwasilisha malalamiko binafsi wakidai Italia imekiuka haki zao za binadamu.

Kamati hiyo hufuatilia masuala ya haki za binadamu kwa nchi ambazo zimetia saini mkataba wa kimataifa kuhusu haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni ambapo Italia iliuridhia mwaka 1978.

Baada ya wenza hao kutafuta matibabu katika moja ya vituo vya uzazi mwaka 2009 , kituo hicho kilizalisha kiini tete ambacho kilikuwa na nafasi ndogo ya kufanikiwa kutengeneza mtoto. Akihofia kwamba ujauzito utatoka na kupoteza mtoto mwanamke huyo aliomba kiini tete hicho kisipandikizwe katika mfuko wake wa uzazi , hata hivyo kliniki hiyo ilimfahamisha kwamba haruhusiwi kukataa kufanya hivyo chini ya sheria namba 40/2004 za nchi hiyo, na wakamtishia kwamba watamshitaki endapo ataendelea kukataa kupandikizwa kiini tete.

Mwanamke huyo akahisi hana chaguo bali kukubali kupandikizwa kiini tete na hatimaye akapoteza ujauzito. Na baada ya mahaka nchini Italia kukataa kusikiliza kesi yao wenza hao wakaamua kuipeleka kwenye kamati ya Umoja wa Mataifa ya haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni ambayo ina wajibu wa kusikiliza malalamiko binafsi kutoka kwa watu ambao hawana chaguo lingine la hatua za kisheria katika nchi zao. Na mwaka 2015 Italia ilitia saini mkataba wa kamati hiyo na hivyo kuipa uwezo wa kufanya maamuzi ya malalamiko yanayowasilishwa dhidi ya Italia.

Mwongozo wa kisheria uliotolewa na kamati hiyo mwaka 2016 unaeleza kwamba “Haki ya ngono na afya ya uzazi ni miongoni mwa haki za uhuru wa mtu. Uhuru huo ni pamoja na haki ya kufanya maamuzi kwa uhuru,  bila ghasia, kutengwa na kubaguliwa, katika masuala yanayohusu mwili , jinsia ya mtu na afya ya uzazi.”

Kwa mujibu wa kamati hiyo sheria ya Italia katika kesi hii imezuia haki ya mwanamke huyo aliyefanyiwa matibabu kubadili nia ya kufanya hivyo na kusababisha kushinikizwa matibabu na hata kubebeshwa ujauzito kwa wanawake wanaosaka tiba ya aina hiyo.

Katika maamuzi yake kamati imeandika “Uwezekano wa athari mbaya kwa wanawake ni mkubwa na kusababisha ukiukwaji wa moja kwa moja wa haki za binadamu za kiafya na utu” ikifafanua kwamba kumlazimisha mwanamke kupandikizwa kiini tete bila ridhaa yake ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika viwango vya kimataifa na katika haki za kijinsia.

Maamuzi ya kamati hiyo yameitaka Italia kuwalipa fidi waathirika , kuhakikisha kwamba wanapata fursa ya matibabu ya kupandikizwa  viini tete (IVF) bila hofu ya shinikizo na kuchukua hatua za msingi kuhakikisha wanawake wote wanafanya maamuzi huru kuhusu matibabu yanayoathiri miili yao na hususan kuhakikisha haki yao ya kubadili nia ya kupandikizwa viini tete, wakisistiza kwamba nchi wanachama wa mkataba huo wanawajibu wa kisheria wa kutekeleza matokeo na maamuzi ya kamati hiyo kuhusu kesi binafsi.