Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake wanaoishi wa HIV wanalazimishwa kuwa tasa na kutoa mimba:UNAIDS

Vipimo vya virusi vya ukimwi.
Public Health Alliance/Ukraine
Vipimo vya virusi vya ukimwi.

Wanawake wanaoishi wa HIV wanalazimishwa kuwa tasa na kutoa mimba:UNAIDS

Afya

Wanawake wanaoishi na virusi vya ukimwi VVU kote duniani wamekuwa wakipambana  kwa miongo ili kutambuliwa haki zao za afya ya uzazi ikiwemo haki ya kuanza familia na kuwa na watoto. Lakini kwa mujibu wa taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na UKIMWI, UNAIDS kumekuwa na mifano mingi ya wanawake hao kulazimishwa kutozaa na kutoa mimba.

Taarifa hiyo iliyotolewa leo na UNAIDS imeongeza kwamba kikao cha 64 cha kamisheni ya hali ya wanawake duniani kitakachomalizika mwezi wa Machi mwaka huu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa nchini Marekani kitakuwa ni kumbusho kwamba miaka 25 iliyopita, serikali zilipitisha azimio la Beijing na jukwaa la kuchukua hatua.

Na serikali hizo ziliafikiana na kuahidi  kutekeleza haki za binadamu za wanawake wote na kulinda na kuhifadhi afya yao ya uzazi na haki zao.

Shirika hilo limesisitiza kwamba haki hizo “ni pamoja na haki ya kuanza familia na kuwa na watoto, haki ya uhuru wa afya ya uzazi na haki ya kupata fursa ya huduma bora ili kusaidia uhuru wa maamuzi ya uzazi na haki ya kupata huduma moraili kusaidia chaguo lao la afya kwa kuzingatia walivyoelimishwa, usalama na hiyari.”

Na hizi ni haki za msingi ambazo shirika hilo linasema zinapaswa kutekelezwa kwa wanawake wote bila kujali hali yao ya VVU, na kuhakikishwa katika mikataba ya kikanda na kimataifa.

Mwaka 2016 mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliazimia kukomesha hali ya watu kulazimishwa kutokuzaa, hususan kuwafanya tasa wanawake wanaoishi na VVU, katika Azimio la kisiasa la kutokomeza UKIMWI.

UNAIDS inasema inatambua ripoti na utafiti kwamba wanawake wanaoishi na VVU wamekuwa waathirika au wanashinikizwa kutozaa na imeahidi kuunga mkono juhudi za kukabiliana na changamoto hiyo kote duniani, UNAIDS na familia ya Umoja wa Mataifa wako tayari kuzisaidia serikali, asasi za kiraia na wadau wengine katika kutekeleza mpango wa kukomesha hali hii.”