Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa Quid mbali ya kuhifadhi mazingira umekuwa mkombozi kwa wanawake Italia:UNFCCC

Ubunifu wa mitindo ya nguo kama hii ya vitambaa vinavyotengenezwa kwa magome ya miti ni moja ya mbinu za kujikwamua kiuchumi
UN News/Matt Wells
Ubunifu wa mitindo ya nguo kama hii ya vitambaa vinavyotengenezwa kwa magome ya miti ni moja ya mbinu za kujikwamua kiuchumi

Mradi wa Quid mbali ya kuhifadhi mazingira umekuwa mkombozi kwa wanawake Italia:UNFCCC

Tabianchi na mazingira

Mradi wa Quid unaoendeshwa na wanawake mjini Verona Italia katika sekta ya fasheni mbali ya kushughulikia changamoto za mabadiliko ya tabia nchi pia umekuwa neema kubwa kwa kuwapa ajira wanawake wenye Maisha duni. 

Hiyo ni sauti ya Anna Fiscale mwanzilishi wa mradi huo wa Quid Progetto akisema lengo lake kubwa ilikuwa ni kuwapa fursa ya ajira wanawake wanaoishi katika hali duni mjini Verona nchini Italia ambao ni karibu asilimia 50 ya wafanyakazi wote wa Quid na pia kuwapa mazingira ya kuwa wabunifu na kushona nguo za kipekee.

Mbali ya kushughulikia changamoto za usawa wa kijinsia mradi wa Quid umekuwa mstari wa mbele kupambana na mbadiliko ya tabianchi, kwani unarejeleza vitambaa vya nguo vya hali ya juu vilivyotupwa na kampuni mbalimbali za mitindo ya nguo na kutengeneza nguo za wanawake zenye ubora wa hali ya juu na kisha kuziuza. Anna anasema waliamua kufanya hivyo kwa sababu, “sekta ya mitindo ya nguo ni sekta inayoshikilia nafasi ya pili duniani kwa kutoa hewa chafuzi, kwa sababu makampuni ya fasheni yanatupa uchafu wote wa vitambaa ambavyo havijatumika na nguo ambazo hazijauzika.”

 Kwa jitihada hizo za kulinda mazingira mwaka 2017mradi huo wa Quid ulijishindia tuzo ya mazingira inayotolewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC.

Kwa wanawake wanaofanya kazi katika mradi huu kama mfungwa wa zamani Maran Carelli hii ni fursa adimu akisema kwamba, “kwangu mimi kazi hii ilikuwa mwanzo mpya baada ya kutumikia kifungo changu. Kwa sababu mfungwa anapotoka jela si rahisi kupata kazi. Quid ilinipa kitu ambacho huenda nisingekipata katika jamii”

Mwanzilishi wa Quid Anna anasema kwa siku za usoni matarajio yake ni kuongeza fursa na ajira zaidi kwa watu wanaotoka katika hali ngumu kwa kuongeza uzalishaji, ushirika mpya na kampuni ya mitindo ya nguo na kufungua maduka mapya ya nguo wanazoshona.