Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jinamizi la ubaguzi wa rangi lawaandama wasichana na wanawake Weusi wanaohitaji huduma za afya: UNFPA

Mtaalamu wa afya akikagua kiwango cha sukari katika damu ya mwanamke mjamzito na mwenye ugonjwa wa kisukari katika Kituo cha Usaidizi wa Kisukari na Endocrinology huko Bahia, Brazili.
© WHO/Panos/Eduardo Martino
Mtaalamu wa afya akikagua kiwango cha sukari katika damu ya mwanamke mjamzito na mwenye ugonjwa wa kisukari katika Kituo cha Usaidizi wa Kisukari na Endocrinology huko Bahia, Brazili.

Jinamizi la ubaguzi wa rangi lawaandama wasichana na wanawake Weusi wanaohitaji huduma za afya: UNFPA

Wanawake

Wanawake na wasichana wenye asili ya Kiafrika wanakabiliwa na "ubaguzi wa kimfumo na wa kihistoria wa unyanyasaji wa rangi katika sekta ya afya katika nchi zote ulimwenguni, na kuwaacha katika hatari kubwa ya kifo wakati wa kujifungua, limeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani nna afya ya uzazi UNFPA.

Natalia Kanem, mkurugenzi mtendaji wa UNFPA katika taarifa yake kuhusu suala hili amesema "Janga la ubaguzi wa rangi linaendelea kwa wanawake na wasichana Weusi barani Amerika, ambao wengi wao ni zao la wathirika wa utumwa." 

Ameongeza kuwa "Mara nyingi, wanawake na wasichana hawa wenye asili ya Kiafrika wananyanyaswa na kudhulumiwa, mahitaji yao hayachukuliwi kwa uzito, na familia zao zinavunjwa moyo na vifo vinavyoweza kuzuilika vya wapendwa wao wakati wa kujifungua. Haki na usawa vitawezekana tu wakati mifumo yetu ya huduma ya afya itawaona wanawake hawa na kuwapa huduma kwa heshima na utu.”

Kuanzia unyanyasaji hadi kunyimwa huduma

Kulingana na UNFPA, unyanyasaji wanaokumbana nao wanawake wenye asili ya Kiafrika wanapopokea huduma za afya ni Pamoja na unyanyasaji wa matusi na kimwili hadi kunyimwa huduma bora na kukataa kutulizwa maumivu.

“Matokeo yake, wanakabiliwa na matatizo mengi wakati wa ujauzito na kuchelewa kwa hatua, ambazo mara nyingi husababisha kifo.” Limeongeza shirika hilo.

Matokeo haya yamo katika ripoti ya “Afya ya mama ya wanawake na wasichana wenye Asili ya Afrika katika bara la Amerika”, iliyoandaliwa kwa ushirikiano na shirika la afya kwa nchi za Amerika PAHO, ushirikiano wa kitaifa wa usawa wa kuzaliwa, na mashirika ya Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF na la masuala ya wanawake UN-Women.

Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa watu wenye asili ya Afrika hukabiliwa naunyanyasaji usio na uwiano katika mazingira ya afya, ambayo baadhi yanatokana na imani zisizo za kisayansi, za kibaguzi na enzi za watumwa ambazo bado zipo katika mafunzo ya matibabu.

Tofauti iliyofurutu ada nchini Marekani

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tofauti hiyo imekithiri zaidi nchini Marekani, ambapo wanawake na wasichana Weusi wana uwezekano mara tatu zaidi wa kufariki dunia wakati wa kujifungua au ndani ya wiki sita baada ya kujifungua ikilinganishwa na wanawake wasio wa asili ya Kiafrika na wasio Wahispania.

Vifo vya uzazi pia vinaendelea bila kujali viwango vya mapato na elimu, huku vifo vya uzazi miongoni mwa wahitimu wa chuo Wamarekani wenye asili ya Kiafrika bado ni mara 1.6 zaidi ya wanawake wa kizungu walio na diploma ya chini ya shule ya upili.

Katika ukanda wa nchi za Amerika, ambako kuna wastani wa watu milioni 209 wenye asili ya Kiafrika, ni nchi 11 tu kati ya 35 zinazokusanya takwimu za afya ya uzazi iliyogawanywa kwa rangi.

Wito wa kushughulikia itikadi ya ubaguzi wa rangi

Ili kukabiliana na hali hiyo na kuokoa maisha, UNFPA imezitaka serikali kukusanya na kuchambua takwimu thabiti za afya iliyogawanywa kwa rangi na kabila.

Pia limetoa wito kwa shule za matibabu kushughulikia itikadi ya ubaguzi wa rangi katika mitaala ya mafunzo na kuzitaka hospitali kuanzisha sera za kukomesha unyanyasaji wa kimwili na matusi unaoathiri wanawake na wasichana wenye asili ya Kiafrika.