Ni wakati wa kukitokomeza Kifuu kikuu-UN

Mwanamke huyu wa Pakistani mwenye TB aliishi kwa miaka mitano bila kugundulika kuwa ana ugonjwa huo kutokana na kushindwa kumudu dola 2 za usafiri kutoka kijijini kwake hadi hospitali ya kiraia mjini Tharparkar.
OCHA
Mwanamke huyu wa Pakistani mwenye TB aliishi kwa miaka mitano bila kugundulika kuwa ana ugonjwa huo kutokana na kushindwa kumudu dola 2 za usafiri kutoka kijijini kwake hadi hospitali ya kiraia mjini Tharparkar.

Ni wakati wa kukitokomeza Kifuu kikuu-UN

Afya

Shirika la afya duniani kupitia taarifa yake ya leo jumapili katika siku ya Kifua Kikuu au TB duniani, linasema ugonjwa huo siyo tu ni ugonjwa wa maambukizi unaoua zaidi duniani kote bali pia ni ugonjwa unaoongoza kusababisha vifo kwa watu wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI, au VVU, pia ndiyo ugonjwa unaosababisha zaidi vifo vinavyotokana na magonjwa ambayo yamekuwa sugu dhidi ya madawa.

Kifua kikuu kwa mujibu wa WHO bado ni ugonjwa wa maambukizi unaoongoza kwa kuua takribani watu 4,500 kila mwaka na unawasumbua watu wengine takribani 30,000 duniani kote.

Tangu mwaka 2000, jitihada za ulimwengu kuutokomeza ugonjwa huu unaozuilika na kutibika, zimeokoa watu wanaokadiriwa kufikia milioni 54 na zimepunguza vifo vitokanavyo na TB kwa asilimia 42. “Kauli mbiu ya siku ya TB duniani mwaka huu inasema ‘Ni wakati wa kuitokomeza TB,’ “anasema Dkt Tedros Adhanos Ghebreyesus, Mkurugenzi mkuu wa WHO ambao wanaongoza kampeni ya ‘Tafuta.Tibu.Wote. #TokomezaTB’

Pamoja na juhudi za jumla za WHO kuelekea kuwa na uhakika wa bima ya afya kwa wote, katika siku hii ya TB duniani, WHO inatoa wito kwa serikali, jamii zilizoathirika, mashirika ya kiraia, watoa huduma za kiafya na wadau wa kitaifa na kimataifa kuunganisha nguvu za pamoja chini ya mwavuli wa “Tafuta. Tibu. Wote. #TokomezaTB” ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.

Ili kusongesha juhudi za kitokomeza TB, wakuu wa nchi walikutana mwezi Septemba mwaka 2018 katika katika mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa na kuweka ahadi madhubuti ya kuutokomeza ugonjwa huu.

“Tunasisitiza umuhimu wa kutafsiri ahadi tulizojiwekea mwaka 2018 katika mkutano wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa katika matendo ili kuhakikisha kila mtu anayehitaji huduma ya tiba ya TB anapata,” amesema mkuu wa WHO.

Wiki iliyopita, WHO ilitoa mwongozo mpya wa kuboresha namna ya kukitibu kifua kikuu kilichosugu kwa dawa, walitoa ushauri ambao ulihusisha hatua za sekta mbalimbali kufuatilia na kufanya mapitio ya maendeleo au hatua, kuweka kipaumbele mipango na utekelezaji wa kupambana na TB; na kikosi kazi cha kuhakikisha ushiriki wenye tija wa jumuiya za kiraia.

Dkt Tereza Kasaeva, mkurugenzi wa programu ya TB ya WHO anasema, “ hii ni hatua ya vitendo ambavyo nchi zinaweza kutumia ili kuharakisha maendeleo na kutenda kuhusu ahadi za mkutano wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu TB uliofanyika mwezi Septemba 2018.”

Wahamiaji wako hatarini zaidi.

Kwa kuwa TB ni ugonjwa wa kuambukiza na kwa njia ya hewa, wahamiaji ni moja ya makundi ambayo yako hatarini zaidi kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na wahamiaji (IOM).

IOM inasema kuwa wahamiaji wengi wanafanya kazi katika mazingira ya hatari, kazi ngumu na wanaishi katika nyumba zilizoko chini ya kiwango. Wengine wanaweza kufungwa katika vizuizi ambavyo vina idadi kubwa ya watu au wanaishi katika kambi za wakimbizi au zile za wakimbizi wa ndani.

Zaidi pia IOM inasema wahamiaji wanakumbana na changamoto za kikwazo cha lugha, uongozi na hata utamaduni katika kuzifikia huduma za kiafya na mara nyingi wanaondolewa katika mfumo wa ulinzi wa kijamii na programu za bima ya afya kwa wote.

"Ni wakati wa kuwajumuisha wahamiaji” IOM inasisitiza.

Kila mwaka tarehe 24 ya mwezi Machi, Dunia inaadhimisha siku ya TB kwa kukuza uelewa kuhusu ugonjwa hu una athari zake kwa afya, jamii na uchumi na pia hatua za kuchukua ili kuutokomeza duniani kote. Hii ni kumbukumbu ya siku ambayo mnamo mwaka 1882, Dkt Robert Koch alitangaza kugundua bakteria anayesababisha TB na hivyo ikafungua njia kuelekea kuugundua ugonjwa na kuyatibu maambukizi haya.