Jumuiya ya kimataifa inawajibika kimaadili kusaidia wasyria-Guterres

16 Machi 2019

Serikali kote ulimwenguni zinawajibika kimaadili kusaidia wasyria kwa ajili ya mustakabali bora na hatimaye kuweka kikomo mzozo wa miaka minane, amesema katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, kupitia taarifa yake iliyotolewa Ijumaa.

“Wakati mzozo wa Syria ukiingia mwaka wa tisa, wasyria wanaendelea kuteseka kutokana na mzozo mbaya zaidi wa zama hizi,” amesema Guterres akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua. “Mamia ya maelfu wameuwawa, wengine wengi wamelemazwa viungo na hata kisaikolojia, mamilioni wanasalia wakimbizi, makumi ya maelfu wamefungiwa na hawajulikani waliko huku mamia ya maelfu wamefariki, na wasyria walioko kaskazini mashariki na kasikazini magharibi wanaishi na hofu ya janga lingine la kibinadamu linalofanyika,” amesema Katibu Mkuu.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati huu ambapo ufadhili wa dola bilioni 7 zimeahidiwa kwa ajili ya nchi hiyo inayoghubikwa na machafuko katika kongamano la mawaziri kimataifa huko Brussels, bwana Guterres ametoa wito, “kwa pande kinzani Syria kuzingatia dhamira yao na makubaliano ya kusitisha ghasia Idlib.”

Kufuatia kuzuka kwa ghasia katika jimbo linaloshikiliwa na waasi, Guterres amesema, “Nina wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti za kuongezeka kwa operesheni za kijeshi katika wiki chache zilizopita. Juhudi za kukabiliana na ugaidi hazipaswi kuingilia jukumu la kulinda raia. Kusitisha makubaliano Idlib ni hatua muhimu kwa ajili ya kufungua njia kwa kutokomezwa machafuko kote nchini,” ameongeza Katibu Mkuu.

Wakati machafuko yakiendelea kushuhudiwa katika kiwango chochote, Guterres amesema kwamba, “sheria ya kimataifa inahitaji kuzingatiwa na haki za binadamu kulindwa. Raia wasio na hatia, wengi wakiwa ni wanawake na watoto, wamelipa gharama kubwa katika mzozo kwa ajili ya kupuuzwa kwa sheria ya kimatifa ya kibinadamu na haki za binadamu.”

Tatu amesema, “uwasilishaji endelevu wa misaada ya kibinadamu ni muhimu kwani watu milioni 11.7 wanamahitaji ya ulinzi na kibinadamu.” Hatimaye ameongeza kuwa akitoa shukrani kwa wafadhili wote walioahidi kutoa msaada wa kifedha mjini Brussels, “kuimarisha msaada wa kimataifa unahitajika haraka iwapo pande husika katika mzozo wataelekea katika kutafuta suluhu ya kisiasa itakayofikia mahitaji muhimu na ndoto za wasyria wote.”

Bwana Guteress amehitimisha kwa kusema kwamba, “ni wajibu wa kimaadili na muhimu kisiasa kwa jamii ya kimataifa kusaidi wasyria na kuungana kwa maono ya mustakabali unaolinda raia, unaondoa madhila, na kuzuia ukosefu wa usalama, unakabiliana na kiini cha mzozo na kutafuta, hatimaye suluhu yenye makubaliano na wote.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter