Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taswira ya wanawake viongozi duniani licha ya hatua haijafikia 50-50-UN

Wanawake na uongozi
UN Women/Ryan Brown
Wanawake na uongozi

Taswira ya wanawake viongozi duniani licha ya hatua haijafikia 50-50-UN

Wanawake

Mkutano wa 63 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani, CSW, ukiwa umeingia siku ya pili kwenye mako makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, hii leo baadhi ya mada ambazo zimejadiliwa ni wanawake na uongozi.

Akizungumza kwenye mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amerejelea kauli yake kwamba usawa wa jinsia kimsingi ni suala la madaraka akiongeza kuwa hiyo ndio sababu anasukuma usawa wa jinsia kwenye Umoja wa Mataifa.

Katibu huyo mkuu akaenda mbali zaidi kuhoji,  “ni kwa nini ni kiungo muhimu, kwa nini tunajizatiti kufungua milango ya fursa kwa wanawake mahiri, wenye uwezo na waliokidhi vigezo? Ndio ni kwasababu ya usawa, kwa sababu ni haki lakini, ni zaidi ya hilo. Tunahitaji usawa wa kijinsia na hebu nirudie tena, kubadili mahusiano ya madaraka katika jamii ili usawa wa kijinsia uwe halisi.”

Bwana Guterres ameongeza kuwa, “tunahitaji pia mabadiliko ya mahusiano ya madaraka ili kusongesha mbele amani na usalama kwa wote kwani usawa wa kijinsia ni kiungo muhimu cha amani na usalama. Kuchagiza haki za binadamu kwani usawa wa kijinsia ni kiini cha haki za binadamu, kuhakikisha maendeleo kwa wote, kwani usawa wa kijinsia ni kichocheo muhimu cha maendeleo. Ukweli ni kwamba wanawake wakiwa katika meza ya majadiliano, uwezekano wa amani endelevu inaongezeka.”

Katibu mkuu amesema wazi kuwa, iwapo dunia itawatenga wanawake, sote tutalipa gharama na tunapowajumuisha wanawake, dunia inashinda,na wote tunashinda.

Kwa upande wake rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Maria Fernanda Espinosa amesema ni muhimu kutambua wanawake ambao walitangulia na ambao “wametuwezesha sote kuwepo duniani leo. Safari ya haki za wanawake imekuwa ndefu, hakuna mafanikio yangefikiwa leo bila ya kupigania kwa haki kwa wanawake wa jamii za asili, wanawake wa asili ya Afrika, wafanyakazi, wanawake wahamiaji, vijana wa kike, wasanii, wanasayansi, wanawake wanaoishi na ulemavu, wanawake wa vijijini na wanawake kutoka sehemu mbali mbali.”

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 73 María Fernanda Espinosa Garcés (kushoto),akiwa katika picha ya pamoja na Kersti Kaljulaid Rais wa Estonia, Katrín Jakobsdóttir waziri mkuu wa Iceland na  Paula-Mae Weekes,Ras wa Trinidad and Tobago baada
Picha na UN/ Mark Garten
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 73 María Fernanda Espinosa Garcés (kushoto),akiwa katika picha ya pamoja na Kersti Kaljulaid Rais wa Estonia, Katrín Jakobsdóttir waziri mkuu wa Iceland na Paula-Mae Weekes,Ras wa Trinidad and Tobago baada

Bi. Espinosa ameongeza kuwa, “tumetoka mbali katika safari ya kupunguza pengo la usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume lakini bado tunavizuizi vingi vya kukabiliana navío pengo nyinig za kuziba na mengi ya kubadilisha.”

Naye mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema, “hapa kwenye Umoja wa Mataifa tumepiga hatua lakini tunaishi katika dunia ambamo kwamo kuna nchi 10 tu ambako kuna uwakilishi sawa wa wanawake katika Baraza la Mawaziri. Asilimia 75 ya wabunge duniani ni wanaume, asilimia 19 tu ya viongozi wa ngazi ya juu wanaongoza nchi zao ni wanawake na asilimia tano tu ya wanawake ni wakurugenzi wakuu katika kampuni 500 za juu kote duniani na idadi hiyo inapungua, hii ni changamoto kubwa na hivyo kuja pamoja kwa namna hii ni fursa ya kutoa wito kwetu sote kusisitiza changamoto iliyopo na kutoa wito kwa ajili ya kuleta mbadiliko.”

Wakati huohuo Umoja wa Mabunge duniani, IPU katika taarifa kwa vyombo vya habari imesema uwakilishi wa wanawake katika viti vya maamuzi vya kisiasa unaongezeka kidogo tangu mwaka 2017 kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa kwenye chapisho la IPU kuhusu ramani ya wanawake katika siasa.

Kwa mujibu wa ramani hiyo ya IPU kufikia tarehe Mosi mwezi Januari mwaka huu wa 2019 idadi ya mawaziri kote ulimwenguni ni ya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa ikiwa ni asilimia 20.7 ambayo ni ongezeko la asilimia 2.4 ikilinganishwa na mwaka 2017.

 

Rais wa IPU akiwa kwenye picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Picha na UN/Photo/Loey Felipe
Rais wa IPU akiwa kwenye picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Rais wa IPU na mbunge kutoka Mexico Gabriela Cuevas Barron, amesema “uwakilishi sawa katika vyeo vya serikali ni muhimu ili kufikia demokrasia kwa wote na yenye athari chanya.Licha ya hatua mujarabu, idadi kubwa ya viongozi wa serikali ni wanume, ni jukumu la pamoja kwa wanaume na wanawake kubadili hili na kuhakikisha usawa wa kijinsi katika siasa.”

Kwa mujibu wa ramani ya IPU nchi tisa zina wanawake asilimia hamsini au zaidi katika Baraza la Mawaziri. Hispania asilimia 64.7, Nicaragua asilimia 55.6, Sweden asilimia 54.4, Albania asilimia 53.3, Colombia asilimia 52.9, Costa Rica asilimia 51.9, Rwanda asilimia 51.9, Canada asilimia 50 na Ufaransa asilimia 50.

Miongoni mwa nchi ambazo zilishuhudia ongezeko la wawakilishi wanawake kaika siasa ni Ethiopia kutoka asilimia 10 mkwa 2017 hadi asilimia 47.6 mwaka 2019.

Mashariki ya kati na Afrika Kaskazini, Mauritania ina idadi kubwa ya wanawake katika ukadan huo ikiwa ni asilimia 31.8 na Muungano wa nchi za kiarabu ukifuata na asilimia 29.

Idadi ya nchi ambazo zisizo na wanawake mawaziri zilipungua kutoka 13 hadi 11 ikiwemo, Azerbaijan, Belize, Brunei Darussalam, Iraq, Kiribati, Lithuania, Papua New Guinea, Saint Vincent and the Grenadines, Saudi Arabia, Thailand na Vanuatu.