Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CSW63 yakunja jamvi kwa mkakati kuwahakikishia wanawake ulinzi, usalama na fursa za kiuchumi.

Washiriki wa CSW63 wakisherehekea kukamilika kwa mkutano huo mjini New York Marekani.
UN Women/Ryan Brown
Washiriki wa CSW63 wakisherehekea kukamilika kwa mkutano huo mjini New York Marekani.

CSW63 yakunja jamvi kwa mkakati kuwahakikishia wanawake ulinzi, usalama na fursa za kiuchumi.

Wanawake

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na kukuza usawa wa kijinsia na kuwaezesha wanawake, UN Women limehitimisha mkutano wake wa mwaka mwishoni mwa wiki hii mjini New York Marekani kwa makubaliano kuhusu njia za kulinda na kuboresha jinsi wasichana na wanawake watakavyoweza kufikia mifumo ya ulinzi wa kijamii, huduma za kijamii na miundombinu endelevu.

Mkutano huo wa 63 wa kutathimini hali ya wanawake duniani CSW63 ambao kwa kawaida unawaleta pamoja wanaharakati wa haki za wanawake kutokakote duniani kuja katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kwa muda wa wiki mbili kufanya majadiliano ya kina, vikao vya wataalamu na vikao vya wadau, umehitimishwa kwa ahadi nzito kutoka kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa za kuhakikisha kuwa huduma, miundombinu na mifumo ya ulinzi wa kijamii inaandaliwa na kutekelezwa kwa njia ambazo zinazuia unyanyasaji na hivyo kuweka uwanja ulio sawa kwa wanawake na wasichana.

[scald=163021:sdl_editor_representation]

Mkurugenzi mtendaji wa UN Women ambaye pia anahudumu kama katibu wa CSW, Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema,“mapendekezo ya tume yanatengeneza njia kwa serikali zote kushiriki na kuwekeza kwa namna tofauti wakiwahusisha wanawake katika mijadala ya kisera, na kulenga mipango ambayo inaenda kwenye kiini cha vikwazo vikuu vya kuwawezesha na kuwapa sauti wanawake na wasichana.”

Mkutano huu wa CSW63 ulianza tarehe 11 Machi kwa hotuba ya mama wa kipakistani anayetumia kitimwendo ambaye anatamani kutembea katika bustani bila kuwa na wasiwasi wa mahali pa kupita, na pia hotuba kutoka kwa mwanamke mdogo kutoka Sudan Kusini ambaye anaota kuwa na huduma nafuu za afya.

Hayo pamoja na shuhuda nyingine kama hizo zimesikika katika kipindi cha wiki hizi mbili za mkutano na vikao wakijadili ukweli kuhusu malipo ya uzeeni, huduma bora za kiafya na huduma za usafiri wa jamii zilizo nafuu namna vinavyoweza kuwasaidia wanawake kuwa na uhakika wa kipato na kuwa huru na vile vile kuweza kuweka mazingira yanayoweza kumfanya mjasiriamali mdogo kuweza kuzifikisha bidhaa zake kwa muda sokoni, na kwa gharama kiasi gani au ni namna gani msichana kigori anavyoweza kwa usalama kufika shuleni kwake na anaweza kupata maliwato ya kujitiri anapohitaji kufanya hivyo.

Hali hii inaweza kuamua pia ikiwa msichana aende shule au la, soko gani mwanamke mkulima aende na ni muda kiasi gani anabakiwa nao kuweza kufanya shughuli nyingine za kujipatia kipato au hata kupumzika.

Matokeo ya mkutano ambayo yanafahamika kama makubaliano ya kuhitimisha yanaeleza kinagaubaga kwa kuweka hatua muhimu za kupaza sauti, uongozi wa wanawake na wasichana kama wanufaika na watumiaji wa mifumo ya usalama wa kijamii, huduma za kijamii na miundombinu endelevu.

Mifumo ya ulinzi wa kijamii, huduma za kijamii na miundombinu endelevu ni muhimu katika kufikia utekelezaji wa azimio la mkutano wa Beijing wa mwaka 1995 na Jukwaa la Kazi na Agenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu iliyopitishwa na viongozi wa dunia mwaka 2015.