Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CSW63 kuanza leo New York, Marekani, mustakabali wa wanawake na wasichana kuangaziwa

Wasichana na ICT huko Juba, Sudan Kusini.
UNDP South Sudan
Wasichana na ICT huko Juba, Sudan Kusini.

CSW63 kuanza leo New York, Marekani, mustakabali wa wanawake na wasichana kuangaziwa

Wanawake

Mkutano wa 63 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani, CSW unaanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ukileta pamoja zaidi ya washiriki 9000 kutoka wawakilishi wa nchi 193 wanachama wa umoja huo pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale ya kiraia.

Mwenyekiti wa mkutano huo wa takribani wiki mbili balozi Geraldine Byrne Narson kutoka Ireland amesema maudhui makuu ni mifumo ya hifadhi ya jamii, upataji wa huduma za umma, miundombinu endelevu kwa ajili ya usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake na wasichana na kwamba mkutano huu ni muhimu zaidi kwa kuwa…
“Masuala kama vile huduma nafuu ya malezi ya watoto, huduma ya afya na elimu, ukosefu wa huduma za hifadhi ya jamii, na usafiri salama na nafuu. Naamini kwa kushughulikia masuala haya ni muhimu kwa ajili ya usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote.”

Balozi Narson amesema kwa kuzingatia maudhui hayo kwa mara ya kwanza kabisa, CSW inachukua hatua muhimu zaidi na kwamba..

“Hatuwezi kupoteza fursa hii wakati huu ambapo tunasubiri maadhimisho ya miaka 25 ya jukwaa la Beijing la hatua za utekelezaji ambalo linapigia chepuo haki za mwanamke ni haki za binadamu.”

Washiriki kwenye mkutano huo, watatathmni pia hitimisho la mkutano wa 60 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani, ambalo lilikuwa uwezeshaji wa wanawake na uhusiano wake na maendeleo endelevu.
Wakati huo huo, ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo wa kamisheni ya hali ya wawanake duniani, utakuwa na matukio ya kando yakilenda maudhui kuu  ya mkutano huo.

Matukio hayo ni miundombinu endelevu kwa usawa wa jinsia siku ya jumanne, mifumo ya Ulinzi wa Jamii siku ya jumatano na uwezeshaji wanawake na wasichana tarehe 20 ya wiki ijayo.