Tusikose lishe kwa kupoteza na kutupa chakula:FAO

7 Novemba 2018

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO limetoa wito wa kuhakikisha chakula hakipotei au kutupwa hovyo ili kulinda virutubisho na lishe muhimu kwa ajili ya maisha ya binadamu.

Kwa mujibu wa FAO wakati mtu mmoja kati ya watano hufariki dunia kwa sababu zinazohusiana na lishe duni, sera iliyozinduliwa leo na shirika hilo inawataka watunga sera kutoa kipaumbele upunguzaji wa kupoteza au kutupa chakula kama njia ya kuboresha fursa ya watu kupata virutubisho na lishe bora.

Sera hiyo “Kuzuia upotevu wa virutubisho na utupaji katika mfumo wa chakula : hatua za kisera kwa ajili ya lishe bora” inabainisha kwamba lishe duni sasa ndio tishio kubwa la afya ya umma kuliko malaria, kifua kikuu au surua.

FAO inasema wakati huohuo takriban theluthi moja ya chakula chote kinachozalishwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu hakimfikii mlaji. Sera hiyo pia inatambua ni jinsi gani vuakula kama matunda , mbogamboga, mbegu, bidhaa za maziwa na samaki vina vitrutubisho vingi, lakini pia ndio vinavyoharibika haraka na hivyo viko hatarini kupotea au kutupwa katika mfumo mzima wa chakula.

Shirika hilo limeongeza kuwa idadi inasikitisha “Kila mwaka zaidi ya nusu ya matunda na mbogamboga zote zinazozalishwa zinapotea au kutupwa. Na vyanzo muhimu vya ptotini, kama asilimia 25 ya yanma zote zinazozalishwa sawa na ng’ombo milioni 75 hawatumiki.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa FAO Jose Graziano da Silver “Ili kukabiliana na aina zote za utapia mlo na kuchagiza lishe bora, tunmahitaji kuweka mifumo ya chakula ambnayo itaongeza upatikanaji, wa gharama nafuu na ulaji wa vyakula vyenye lishe bora kwa wote. Kuchukua hatua madhubuti kupunguza upotevu wa lishe bora ni sehemu muhimu sana ya juhudi hizi.

Hatua za kuchukuliwa katika mfumo wa chakula

Sera hiyo inapendekeza kuchukuliwa hatua kadhaa za kisera katika mfumo wa chakula ikiwemo :kuelimisha wadao wote, kujikita katika vyakula vinavyoharibika haraka , kuboresha miundombinu ya umma na binafsi, kuchagiza ubunifu na kuziba mapengo ya takwimu na ujuzi kuhusu upotevu na utupaji wa chakula. 

Takwimu za FAO zinaonyesha kwamba katika nchi za kipato cha chini chakula mara nyingi hupotea wakati wa mavuno , uhifadhi, utayarishaji na usafirishaji , wakati katika nchi za kipato cha juu tatizo ni moja la upotevu wa chakula katika kiwango cha uuzaji na walaji. Na kwa pamoja vinaathiri lishe ambayo inahitajika kutumiwa kwa afya za watu.

Kimataifa kilimo kinazalisha asilimia 22 zaidi ya vitamini A kuliko inavyohitajika, hatahivyo baada ya utupaji na upotevu wa chakula kiwango kinachopatikana kwa matumizi ya binadamu ni asilimilia 11 au pungufu kuliko inavyohitajika.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter