Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Venezuela: Rasimu ya Marekani  yapigwa turufu, ya Urusi yapingwa

Taswira ya ukumbi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa kikao kuhusu hali ilivyo nchini Venezuela
UN/Eskinder Debebe
Taswira ya ukumbi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa kikao kuhusu hali ilivyo nchini Venezuela

Venezuela: Rasimu ya Marekani  yapigwa turufu, ya Urusi yapingwa

Amani na Usalama

Kwa mara nyingine tena wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameendelea kutunishiana misuli kuhusu suala la Venezuela ambapo hii leo vuta ni kuvute imeendelea tena ndani ya baraza wakati maazimio mawili yaliyowasilishwa kwa lengo la kusaka suluhu ya mzozo unaoendelea kwenye taifa hilo la Amerika ya Kusini yalipogonga mwamba.

Eliott Abrams, Mwakilishi maalum wa Marekani kuhusu  Venezuela, akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali nchini Venezuela
UN / Evan Schneider
Eliott Abrams, Mwakilishi maalum wa Marekani kuhusu Venezuela, akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali nchini Venezuela

Maazimio hayo lile nambari 186 lililowasilishwa na Marekani na lile nambari 190 lililowasilishwa na Urusi yote yalipigiwa kura lakini hakuna hata moja ambalo lilipata kura za kutosha ili liweze kutekelezwa.

Azimio lililowasilishwa na Marekani pamoja na mambo mengine linaeleza kuwa uchaguzi wa mwezi Mei mwaka 2018 uliomweka madarakani Rais Nicolas Maduros haukuwa huru na haki na hivyo linataka uchaguzi mpya ufanyike.

Wajumbe walipiga kura ambapo wajumbe 9 walisema ndio, 3 walisema hapana na 3 hawakuonyesha msimamo wowote.

Ingawa lilipata kura 9 kati ya wajumbe 15 wa Baraza hilo,  halikuweza kupita kwa kuwa Urusi na China ambazo ni wajumbe wa kudumu walipiga kura ya hapana na kura zao ni turufu.

Kwa upande wake, azimio lililowasilishwa na Urusi linaonyesha wasiwasi wake kuhusu vitisho ya kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya taifa huru na majaribio ya kuingilia masuala ya ndani  ya nchi.

Kura ilipopigwa, wajumbe  4 walisema ndio, 7 walisema hapana na 4 hawakuonyesha msimamo wowote, na halikupita kwa sababu ya kura hazikutosha.

Vuta nikuvute hiyo inaendelea ilhali vifo na majeruhi wameripotiwa kwenye sakala linaloendelea nchini humo.

Misimamo ya wajumbe baada ya kupiga kura

Wakichangia misimamo yao ya upigaji kura, Marekani imeelezea masikitiko yake ikisema matokeo ya kura dhidi ya rasimu yake ya azimio ni kiashiria ya jinsi wajumbe wa Baraza la Usala wanaendelea kushamirisha utawala wa Rais Maduros.

China imesema imepinga azimio lililowasilishwa na Marekani kwa kuzingatia kuwa linaingilia masuala ya ndani ya taifa huru na hivyo ni lazima kusaka suluhu kwa misingi ya kikatiba.

Kwa upande wake Urusi imesema suala la kutaka uchaguzi mwingine ufanyike kwa madai ule wa mwaka jana haukuwa huru na haki, takribani mwaka mmoja tangu ufanyike, ni suala ambalo halina mashiko yoyote.

Vassily Nebenzia, Mwakilishi wa kudumu wa  Urusi kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Venezuela
UN/Eskinder Debebe
Vassily Nebenzia, Mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Venezuela

Afrika Kusini yastaajabu msimamo wa Baraza

Nayo Afrika Kusini kupitia mwakilishi wa kudumu wa Afrika Kusini kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Jerry Matthews Matjila imesema kimsingi inaunga mkono jitihada za Umoja wa Mataifa za kusaka suluhu ya kibinadamu kwenye mzozo wa Venezuela.

Hata hivyo amesema kitendo cha kuwepo kwa rasimu mbili za maazimio zinazokinzana ni kiashiria tosha cha kutokuwepo kwa muungano wa Baraza la Usalama katika kutekeleza jukumu lake la amani na usalama duniani.

“Badala ya baraza hili kuungana na kuleta watu pamoja, linagawanyika na kudidimiza uwezo wake wa kutekeleza jukumu lake. Linapaswa kuibuka na azimio moja,” amesema Balozi Matjila.

Venezuela yafunguka: Hatua mzozo wowote, kama upo  unaletwa na wageni

Akitamatisha mjadala, mwakilishi wa kudumu wa Venezuela kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Samuel Moncada, amesema kuwa Venezuela iko kwenye amani kutokana na uongozi wa Rais Maduros.

Amesema tishio lolote la amani kama lipo linatoka nje ya nchi na si ndani.

Samuel Moncada, Mwakilishi wa kudumu wa Venezuela  kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama la UN
UN /Manuel Elias
Samuel Moncada, Mwakilishi wa kudumu wa Venezuela kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama la UN

Akizungumzia rasimu ya azimio lililowasilishwa na Marekani, Balozi amesema hakuna taifa lolote lenye mamlaka ya kuamua mchakato wa kidemokrasia wa taifa lingine. "Marekani na Ulaya si watawala wa dunia," ameongeza Balozi Moncada akidai kuwa wale wanaojidai wana huruma na Venezuela wana ajenda zao.

Hii ni mara ya tatu kwa Baraza la Usalama kukutana na kujadili sakata la Venezuela katika kipindi cha mwezi mmoja.

Sakata la Venezuela lilianza baada ya Rais Nicolas Maduros kuapishwa kuongoza Venezuela kwa kipindi cha miaka 6 kufuatia uchaguzi wa mwaka jana huku mpinzani wake Juan Guaidó, kupinga na kutaka aondoke madarakani.