Fahamu kwa kina msimamo wa UN na sakata la Venezuela

13 Februari 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali inayoendelea hivi sasa nchini Venezuela ambako kuna mvutano kati ya serikali ya Rais Nicolas Maduros na kiongozi wa upinzani Juan Guaidó.

Bwana Guterres alieleza wasiwasi huo wakati wa mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, Jorge Arreaza uliofanyika Jumatatu jijini New York, Marekani kufuatia ombi la waziri huyo.

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema ofisi yake iko tayari kutoa msaada iwapo pande zote mbili zitaazimia kuwa na mashauriano makini la kufanikisha suluhisho la amani.

Kuhusu iwapo wawili hao wamejadili hali ya kibinadamu nchini Venezuela, Umoja wa Mataifa umesema ni kweli wamejadili hali ya kiuchumi na kijamii.

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema, “kwa kuzingatia mkwamo wa sasa, inakuwa ni dhahiri shairi kuwa mashaurino ya kina ya kisiasa kati ya pande mbili hizo ni muhimu ili kupata suluhu itakayowezesha amani ya kudumu kwa wananchi wote wa Venezuela.

UNHCR/Santiago Escobar-Jaramillo
Wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela wakivuka mpaka kuingia Comombia mnamo tarehe 16 Oktoba 2018

Je kuna uwezekano wa kuteua mratibu wa kibinadamu kwa Venezuela?

Umoja wa Mataifa umesema hakuna uteuzi rasmi wa mradi wa kibinadamu kwa Venezuela. Waratibu wote wakazi hufanya kazi na serikali na taasisi ili kushughulikia mahitaji ya wananachi kwenye nchi ambazo wanahudumia.

Hata hivyo Umoja wa Mataifa umesema ukotayari kuongeza shughuli zake huko Venezuela kwenye maeneo ya msaada wa kiufundi na maendeleo.

Je Umoja wa Mataifa unahusika na ukusanyaji na usambazaji wa misaada ya kibinadamu huko Cucuta, Colombia kwa ajili ya Venezuela?

© UNHCR/Luiz Fernando Godinho
Watu 233 kutoka Venezuela waondoka Boa Vista katika awamu ya pili ya utaratibu wa kuwahamisha ambapo waomba hifadhi kutoka Venezuela wanawasili katika miji karibu na mipaka wanoahmishwa maeneo mengine ya Brazil. Aprili 5, 2018

Umoja wa Mataifa umesema hauhusiki na ukusanyaji au usambazaji wa misaada inayoandaliwa na Colombia.

Badala yake umesema misaada ya kibinadamu huangalia mahitaji na hufanyika kwa kuzingatia misingi ya kibinadamu, kutoegemea upande wowote na uhuru. Halikadhalika hatua zozote za kibinadamu hazina uhusiano na upande wowote wa kisiasa, kijeshi au malengo yoyote yale.

Je Umoja wa Mataifa utashiriki kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu Venezuela?

Umoja wa Mataifa umesema hauna taarifa kuhusu mkutano huo.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

UM hauegemei kundi lolote katika sakata la Venezuela:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amesema kuhusu hali ya Venezuela kuna hatua kadhaa zilizoanzishwa na makundi mbalimbali katika kusaka suluhu ya mgogoro unaoendelea nchini humo.

Sakata la Venezuela: Katibu Mkuu hana mamlaka ya kutambua au kutotambua taifa au kiongozi wake- Dujarric

Wakati vuta nikuvute ikiendelea nchini Venezuela kati ya Rais Nicolas Maduros na Juan Guaidó aliyejitangaza kuwa rais wa nchi hiyo, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema kuwa Katibu Mkuu hana mamlaka ya kueleza kukubali au kukataa nchi mwanachama au kiongozi wake.