Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia zashamiri Venezuela, raia 4 waripotiwa kuuawa

Wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela wakivuka daraja la Simon Bolivar nchini Veneuela.
UNHCR/Siegfried Modola
Wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela wakivuka daraja la Simon Bolivar nchini Veneuela.

Ghasia zashamiri Venezuela, raia 4 waripotiwa kuuawa

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa umeelezea masikitiko yake makubwa kufuatia ghasia zinazoendelea kwenye mpaka wa Venezuela na mataifa ya Brazil na Colombia na ndani ya Venezuela kwenyewe ambapo sasa zimeripotiwa kusababisha vifo na majeruhi miongoni mwa raia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake mjini New York, Marekani ametaka ghasia hizo ziepukwe kwa gharama yoyote ile na silaha za sumu zisitumike dhidi ya raia. 

Amesihi pande zote kupunguza mvutano na wasake juhudi za kuepusha kuimarika zaidi kwa kile kinachoendelea.

Naye Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet naye amelaani kile alichoita, "matumizi ya nguvu kupita kiasi kunakofanywa na majeshi ya Venezuela na ushiriki wa vikundi vinavyounga mkono serikali kwenye mashambulizi dhidi ya raia ambako kumesababisha vifo vya raia wanne na zaidi ya 300 walijeruhiwa katika tukio la ijumaa na jana jumamosi."

Amesema watu wanapigwa risasi na kuuawa na wengine wameripotiwa kupata majeraha ambayo hawatapona maishani ikiwemo kupoteza macho.

"Taswira kama hizi zinachukiza. serikali ya Venezuela lazima izuie majeshi yake yasitumie nguvu kupita kiasi dhidi ya raia wasiokuwa na silaha yoyote," amesema Bi. Bachelet.

Kamishna huyo mkuu wa haki za binadamu amesema amepokea ripoti za matukio ya ghasia kwenye mpaka wa Venezulea na Colombia na Brazil wakati majeshi ya Venezuela yalipojaribu kuzuia misaada isiingine nchini humo.

Halikadhalika amesema ofisi yake imepokea ripoti za mashambulizi dhidi ya raia yanayofanywa na vikundi vinavyounga mkono serikali.

"Nasihi serikali ishikilie makundi haya na wahusika wakamatwe." amesema Bi. Bachelet.

Bi. Bachelet amesema kitendo cha kutumia vikundi vya kando kwenye matukio kama haya ni mambo ambayo yamekuwa yanafanyika na inatia hofu kuwa vikundi hivyo vinatumika kwa uwazi kabisa Venezuela

Amesema serikali inaweza na lazima ivizuie ili visizidi kufanya hali kuwa mbaya zaidi.

Mzozo Venezuela ulianza baada ya Rais Nicolas Maduro kuapishwa kuendelea kuongoza taifa hilo huku mpinzani wake akipinga na kutaka aondoke madarakani.