Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 700 ikiwemo watoto wamezuiliwa kufuatia maandamano Venezuela

Mkimbizi kutoka Venezuela akiwa kwenye daraja la kimataifa la Rumichacha ambalo ni kituo cha kuingilia Ecuador kupitia Colombia. Mwezi novemba mwaka 2018, wavenezuela 2,500 walijaribu kuingia Colombia kupitia mpaka huu.
UNHCR/Santiago Escobar-Jaramillo
Mkimbizi kutoka Venezuela akiwa kwenye daraja la kimataifa la Rumichacha ambalo ni kituo cha kuingilia Ecuador kupitia Colombia. Mwezi novemba mwaka 2018, wavenezuela 2,500 walijaribu kuingia Colombia kupitia mpaka huu.

Watu 700 ikiwemo watoto wamezuiliwa kufuatia maandamano Venezuela

Amani na Usalama

Takriban watu 850 wamezuiliwa nchini Venezuela wakati huu kunaposhuhudiwa maandamano dhidi ya serikail ambapo makabiliano na vikosi vya usalama yamesababisha vifo kwa watu 40 kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo msemaji wa OHCHR, Rupert Colville amesema kuwa watu takriban 700 wamekamatwa katika kipindi cha siku moja, “kulikuwa na takriban watu 696 ambao walikamatwa siku ya Jumatano wiki iliyopita kote nchini. Mawakili wanapokea taarifa ambazo zinathibitisha madai hayo. Hii ndio idadi kubwa ya watu kukamatwa kwa siku moja kwa karibu miaka ishirini iliyopita”.

Kwa mujibu wa OHCHR miongoni mwa waliokamatwa ni Watoto 77 ikiwemo Watoto walio na umri wa miaka 12. Hali hii inafanyika wakati kukishuhudiwa mzozo wa kiuchumi katika nchi hiyo ya Amerika Kusini na kulazimu watu takriban milioni 3 kuondoka Venezuela katika miaka ya hivi karibuni.

Bwana Juan Guaidó ambaye ni kiongozi wa upinzani, tarehe 23 mwezi huu alijitangaza kuwa rais wa muda wa Venezuela, ili hali Rais Nicolas Maduros aliapishwa rasmi kuendelea na wadhifa wa urais kufuatia uchaguzi uliofanyika nchini humo mwezi Mei mwaka jana.

Marekani kwa upande wake imeweka vikwazo vya kiuchumi kwa kuzuia ufikiaji wa mapato kutokana na mauzo ya mafuta.

Janga la kisiasa linaloshuhudiwa kwa sasa limesababisha watu kufurushwa makwao na limekuwa likiongezeka, na tangu 2014 watu milioni 3wamefungasha virago na kukimbia Venezuela.