Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sakata la Venezuela: Katibu Mkuu hana mamlaka ya kutambua au kutotambua taifa au kiongozi wake- Dujarric

Stéphane Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa
Picha ya UN/Jean-Marc Ferré
Stéphane Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa

Sakata la Venezuela: Katibu Mkuu hana mamlaka ya kutambua au kutotambua taifa au kiongozi wake- Dujarric

Amani na Usalama

Wakati vuta nikuvute ikiendelea nchini Venezuela kati ya Rais Nicolas Maduros na Juan Guaidó aliyejitangaza kuwa rais wa nchi hiyo, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema kuwa Katibu Mkuu hana mamlaka ya kueleza kukubali au kukataa nchi mwanachama au kiongozi wake.

Dujarric amesema hayo leo akijbu swali la mwandishi wa habari wakati wa mkutano wake na wanataalamu hao jijini New York, Marekani ambapo aliulizwa iwapo Katibu Mkuu anaweza kuamua kufanya kazi na Bwana Guaidó.

Badala yake Bwana Dujarric amesema, “utambuzi wa kiongozi wa serikali au taifa ni suala la nchi wanachama. Hatujapokea taarifa yoyote ya kwamba kumekuwepo na mabadiliko ya serikali nchini Venezuela. Hiyo inapaswa kuwasilishwa kupitia ujumbe wa kudumu wa nchi husika na hadi sasa hakuna mabadiliko yoyote.”

Amesisitiza kuwa wao wanafanya kazi kila siku na ujumbe wa kudumu wa Venezuela kwenye Umoja wa Mataifa na timu ya umoja huo iliyoko Venezuela inaendelea kufanya kazi za misaada ya kibinadamu kwa kushirikiana na serikali.

Mkimbizi kutoka Venezuela akiwa kwenye daraja la kimataifa la Rumichacha ambalo ni kituo cha kuingilia Ecuador kupitia Colombia. Mwezi novemba mwaka 2018, wavenezuela 2,500 walijaribu kuingia Colombia kupitia mpaka huu.
UNHCR/Santiago Escobar-Jaramillo
Mkimbizi kutoka Venezuela akiwa kwenye daraja la kimataifa la Rumichacha ambalo ni kituo cha kuingilia Ecuador kupitia Colombia. Mwezi novemba mwaka 2018, wavenezuela 2,500 walijaribu kuingia Colombia kupitia mpaka huu.

Alipoulizwa iwapo wamepokea barua kutoka kwa Guaidó ya kuomba msaada kibinadamu, Bwana Dujarric amesema, “tumeona chapisho kwenye mtandao wa twitter likiwa limejumuisha hiyo barua. Tutathibitisha uhalali wake na majibu yatazingatiwa.”

Bwana Guaidó ambaye ni kiongozi wa upinzani, tarehe 23 mwezi huu alijitangaza kuwa rais wa muda wa Venezuela, ilhali Rais Maduros aliapishwa rasmi kuendelea na wadhifa wa urais kufuatia uchaguzi uliofanyika nchini humo mwezi Mei mwaka jana.

Tayari Marekani na mataifa mengine ya Amerika ya Kusini yametangaza kumtambua Bwana Guaidó, huuku Muungano wa Ulaya ukitaka Rais Maduros aitishe upya uchaguzi huru na wa haki la sivyo nao watachukua hatua kwa mujibu wa kipengele namba 233 cha katiba ya Venezuela kinachotambua uwepo wa Kaimu Rais.

Hata hivyo Urusi na mataifa mengine kama vile Afrika Kusini na Equatorial Guinea zimesema suala la Venezuela ni suala la ndani ya nchi hiyo na halipaswi kuingiliwa.

TAGS: Venezuela, Stephane Dujarric,