Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali wanayoishi Watoto Rukban haikubalika katika karne ya sasa-UNICEF

Watoto wakiwa katika kambi ya Rukban nchini Syria. Ni wakimbnizi wa ndabni mwa nchi.
WFP
Watoto wakiwa katika kambi ya Rukban nchini Syria. Ni wakimbnizi wa ndabni mwa nchi.

Hali wanayoishi Watoto Rukban haikubalika katika karne ya sasa-UNICEF

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema watoto katika makazi ya muda ya Rukban kusini mwa Syria mpakani na Jordan wanaishi katika hali mbaya isiyokubalika katika karne hii ya 21.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na UNICEF, watoto wanaendelea kukabiliwa na baridi kali  huku wakikosa mahitaji muhimu yanayohitajika kwa ajili ya malezi ya mtoto ikiwemo huduma msingi ya afya, elimu na ulinzi. Takriban watoto wachanga nane wamefariki Rukban tangu Disemba mwaka jana 2018.

UNICEF licha ya kukaribisha msafara wa misaada ya kibindamu wa hivi karibuni uliowasilishwa katika eneo hilo bado inasema kuwa misaada hiyo haitoshi.

Kwa mantiki hiyo UNICEF imetaka pande husika kwenye mzozo ziwajibike kutafuta suluhu ya kudumu kumaliza madhila ya miaka mingi yanayowakumba watoto. Halikadhalika shirika hilo limesema iwapo pande husika hazitapata suluhu endelevu kwa ajili ya watoto, UNICEF imetoa wito kwa pande hizo kuruhusu ufikiaji wa watoto kwa ajili ya kuwasilisha misaada ya kibinadamu na huduma na ulinzi ambavyo vinahitajika haraka.

Aidha UNICEF imesema, “upatikanaji wa huduma za kuokoa maisha, elimu na ulinzi havipaswi kutumiwa kwa ajili ya manufaa ya kisiasa. Na watoto wa Rukban wanastahili mengi zaidi.”