Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunahitaji zaidi ya dola milioni 900 kwa ajili ya mgogoro wa Rohingya 2019:UN

Bangladesh, wakimbizi warohingya waliokimbia Myanmar kusaka usalama Cox's Bazar
© UNHCR/Santiago Escobar-Jaramillo
Bangladesh, wakimbizi warohingya waliokimbia Myanmar kusaka usalama Cox's Bazar

Tunahitaji zaidi ya dola milioni 900 kwa ajili ya mgogoro wa Rohingya 2019:UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wao mashirika yasityo ya kiserikali, NGOs leo wamezindua mpango wa pamoja (JRP) kwa ajili ya kukabiliana na mgogoro wa Rohingya kwa mwaka huu wa 2019.

Mpango huo unaambatana na ombi la dola milioni 920 ili kukidhi mahitaji ya wakimbizi zaidi ya laki 9 kutoka Myanmar na wengine 330,000 kutoka jamii za Bangladesh zinazohifadhi wakimbizi hao.

Msaada muhimu na huduma kama chakula, maji, usafi na malazi vinachukua zaidi ya nusu ya mahitahi ya fedha ya mwaka huu.Masuala mengine yanayohitaji fedha zilizoombwa yanajumuisha masuala ya afya, makazi, ulinzi ikiwemo wa watoto na kushughulikia masuala ya ukatili wa kingono na ukatili mwingine wa kijinsia, elimu na lishe.

Zaidi ya wakimbizi 745,000 wa Rohingya wamekimbia kutoka Myanmar kwenye jimbo la Rakhine na kuingia Bangladesh tangu Agosti 2017 wakihepa machafuko nchini Myanmar na kujiunga na wakimbizi wa ndani takriban 200,000 katika eneo la Cox’s Bazar ambao walikimbia machafuko ya awali.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na la uhamiaji , IOM, kwa ukarimu wa msaada wa mamlaka ya Bangladesh na jamii ambao walikuwa wa kwanza kusaidia katika hali hiyo ya dharura mahitaji mengi ya msingi yalifanikiwa na maisha ya wengi kuokolewa.

Akizungumzia ukarimu huo mkurugenzi mkuu wa IOM António Vitorino amesema “Mshikamano ulioonyeshwa na serikali ya Bangladesh na uwajibikaji wa washirika wa misaada ya kibinadamu vilihakikisha utekelezaji wa awamu ya kwanza ya pamoja ya huduma mwaka 2018. Sasa katika kusonga mbele tunarejea ahadi yetu ya kutimiza mahitaji ya lazima kwa umma na kuitaka jumuiya ya kimataifa kusaidia juhudi hizo.”

Naye Kamishina Mkuu wa wakimbizi na mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi amesema “Lengo letu la kiutu leo hii ni kukabiliana na tatizo la kutokuwa na utaifa la wakimbizi wa Rohinya na jamii zinazowahifadhi nchini Bangladesh.Tunatumai kwa wakati unaotarajiwa na kwa michango tutaweza kukidhi lengo hilo kupitia ombi la fecha la mwaka huu.”

Ameongeza kuwa wakati tukikidhi mahitaji haya ya lazima ya kibinadamu tunapaswa kutopoteza muelekeo wa kusaka suluhu ya kudumu ya tatizo la wakimbizi wa Rohingya. Amerejea wito wake kwa serikali ya Myanmar kuchukua hatua kushughulikia mizizi ya mgogoro huu ambao umekita mizizi kwa muongo sasa, ili watu wasiendelee kufurushwa kutoka makwao na waliokimbia hatimaye waweze kurejea nyumbani kwa usalama na ut una kuisaidia Myanmar katika ujenzi mpya. Pia amezichagiza nchi katika kanda hiyo na kwingineko kushikamana na Bangladesh na kuisaidia Myanmar kuanza kuweka mazingira bora ya wakimbizi kurejea nyumbani kwa hiyari.