Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 3,000 waingia Mexico kutokea Guatemala siku 14 zilizopita

 Watoto ni miongoni mwa wahamiaji kutoka Amerika ya Kati ambao wanatembea kwa miguu kuelekea mpaka wa Marekani. Hapa waonekana wakiwa katika barbara za Tapachula, Chiapas, Mexico.
UNICEF México
Watoto ni miongoni mwa wahamiaji kutoka Amerika ya Kati ambao wanatembea kwa miguu kuelekea mpaka wa Marekani. Hapa waonekana wakiwa katika barbara za Tapachula, Chiapas, Mexico.

Watoto 3,000 waingia Mexico kutokea Guatemala siku 14 zilizopita

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya watu 12,000 wakiwemo watoto 3000 wameingia Mexico wakitokea Guatemala kati ya tarehe 17 mwezi huu hadi leo, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

UNICEF imetoa taarifa hizo leo mjini New York, Marekani na Mexico City nchini Mexico baada ya ziara ya siku mbili kwenye eneo hilo iliyofanywa na  mkurugenzi wake wa mawasiliano Paloma Escudero.

Akiwa kwenye kituo cha uhamiaji cha Tapachula nchini Mexico, ambacho kinashikilia takribani watu 1,000 wakiwemo wanaume, wanawake na watoto, Bi. Escudero amezungumza na wasichana na wazazi ambao wanashikiliwa kwenye kituo hicho wakisubiri majibu ya hifadhi nchi  nyingine au kurejeshwa nyumbani.

Amesema, “ijapokuwa Mexico inaendelea kwa kiasi kikubwa kutekeleza hatua za kulinda haki za watoto wanapokuwa wanasubiri majibu ya maombi yao ya hifadhi kwenye nchi nyingine, bado kuna changamoto.

Bi. Escudero amesema ni muhimu zaidi kuhakikisha watoto hao wanalindwa hususan wale wanaosafiri pekee yao.

Hata hivyo ameshukuru serikali ya Mexico na watu wake akisema wamekuwa wakarimu kwa maelfu ya watoto na familia zinazovuka mpaka kila uchao kutoka Tecun Uman, Guatemala, kuingia Tapachula, Mexico.

Amesema  bila kujali iwapo watoto hao wanasalia Mexico au wanaendelea na safari kuelekea kaskazini mwa nchi hiyo, ni muhimu wanakuwa na familia zao, hawawekwi korokoroni na kwamba maslahi yao yanalindwa wakati wote wa safari.

Takwimu za serikali ya Mexico zinaonyesha kuwa zaidi ya watoto 30,000 kutoka Honduras, Guatemala na El Salvador walishikiliwa kwa muda mfupi korokoroni nchini Mexico mwaka 2018.

Serikali mpya ya Mexico imetangaza rasmi kuachana na kitendo cha kuwashikilia korokoroni watoto wote wahamiaji na sasa inafanya kazi kutekeleza sera hiyo ambapo  UNICEF na mashirika mengine wanasaidia kwa karibu juhudi hizo.