Skip to main content

Siku ya elimu duniani, UNESCO yasema mwamko katika ushirikiano kimataifa wahitajika kufanikisha SDG4

Siku ya kimataifa ya elimu na tarehe 24 Januari mwaka 2019, ni mara ya kwanza siku hii inaadhimishwa kufuatia Baraza Kuu la UN kupitisha azimio mwezi Disemba mwaka jana.
UNESCO
Siku ya kimataifa ya elimu na tarehe 24 Januari mwaka 2019, ni mara ya kwanza siku hii inaadhimishwa kufuatia Baraza Kuu la UN kupitisha azimio mwezi Disemba mwaka jana.

Siku ya elimu duniani, UNESCO yasema mwamko katika ushirikiano kimataifa wahitajika kufanikisha SDG4

Utamaduni na Elimu

Leo Januari 24 ni siku ya kimatifa ya elimu duniani ambayo inaadhimishwa kwa mara ya kwanza tangu kupitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Desemba mwaka jana kwa kutambua umuhimu wa elimu katika kubadili dunia na kufikia ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu.

Katika ujumbe wake kwa siku ya leo Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, Audrey Azoulay amesema bila elimu jumuishi na sawa na fursa za kudumu kwa wote, nchi hazitafanikiwa kuvunja mzunguko wa umaskini ambao unawaacha nyuma mamilioni ya watoto, vijana na watu wazima.

Bi. Azoulay amesema, “hatutaweza kupata mafanikio katika kukabailiana na mabadiliko ya tabiacnhi, kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kufikia usawa wa kijinsia bila dhamira ya kisiasa kuhusu elimu kwa wote.”

Ameongeza kuwa, “siku ya leo ni muhimu katika kusisitiza mambo muhimu, mosi, elimu ni haki ya binadamu, jambo nzuri kwa umma na wajibu wa umma. Pili elimu ni moja ya nguvu iliyopo mikononi mwetu kuhakikisha huduma za afya, kuimarisha ukuaji wa kiuchumi, kuzindua uwezo na ubunifu tunaohitaji kwa ajili ya kujenga jamii zilizo na stahamala zaidi na endelevu. Mwisho, tunahitaji kutoa wito kwa pamoja kwa ajili ya kuchukua hatua kimataifa.

Watoto wakimbizi nchini Nigeria wakiwa darasani kwenye kambi ya wakimbizi wa Minawao nchini Cameroon
UNHCR/Gaelle Massack
Watoto wakimbizi nchini Nigeria wakiwa darasani kwenye kambi ya wakimbizi wa Minawao nchini Cameroon

Takwimu zinaonyesha changamoto zilizopo kwani watoto milioni 262 na vijana hawahudhurii shule; watoto milioni 617 na barubaru hawawezi kusoma au kufanya hesabu rahisi ambapo chini ya asilimia 40 ya watoto wa kike waliopo kusini mwa  jangwa la Sahara ndio wanahitimu elimu ya sekondari huku watoto milioni 4 na barubaru wakimbizi hawahudhuri shule kwasababu ya mizozo.

Mkurugenzi mkuu huyo amesema, “kwa sababu dunia haipo katika njia sahihi kufikia lengo namba nne la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, tunahitaji mwamko katika ushirikiano kimataifa na hatua za pamoja. Changamoto yetu ni kuhakikisha kuwa elimu inamfaa kila mmoja kwa kuchagiza ujumuishwaji na usawa katika kila nyanja, kuhakisha hakuna anayeachwa nyuma”.

Kwa mantiki hiyo ameongeza kuwa hali hii inamaanisha kuweka juhudi mahsusi kulenga watoto wa kike, wahamiaji watu waliofurushwa nwa wakimbizi; kuwasaidi walimu na kuhakikisha elimu na mafunzo vinazingatia jinsia.

UNESCO imetoa wito kwa serikali kuweka elimu kama kipaumbele kwa kusema, “sisi sote ni washikadau kwenye elimu, hebu tuchukue hatua pamoja kufikia malengo”.