Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhifadhi bora wa sauti na picha ni hazina kubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo-UNESCO

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakiwa wanakagua moja ya filamu za kihistoria zilizohifadhiwa kwenye maktaba ya kumbukumbu ya chombo hicho. (Picha hii ni ya Novemba 2004)
UN /Mark Garten

Utamaduni na Elimu

Urithi wa sauti na picha ni sehemu muhimu ya urithi wetu wa kitamaduni, amesema Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO Bi. Audrey Azoulay katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya urithi wa sauti na picha hii leo.

Katika ujumbe wake uliojikita katika kueleza umuhimu wa kuenzi kumbukumbu za sauti na picha bi Azoulay amesema taswira na sauti zilizorekodiwa katika filamu, video na kanda zinaleta historia ya wanadamu katika maisha ya sasa na kuonesha mkusanyiko wa matukio ya kumbukumbu, hali ambayo amesema bila vyombo hivi matukio hayo yangepotea katika kumbukumbu au yangesalia katika mfumo usio na mtiririko.

“Urithi wa sauti na picha ni chanzo kikubwa cha ujuzi na ushuhuda wa utofauti wetu wa kijamii, utamaduni na lugha,” ameeleza mkurugenzi huyo wa UNESCO akiongeza kwamba “kumbukumbu hii, ambayo imesalia hai na ni muhimu kwa wanahistoria, wanasayansi na wananchi wa kawaida wanatafuta ujuzi wa siku za nyuma, hata hivyo ni tete.”

Amesema urithi huo unatishiwa na ukosefu wa teknolojia na vyombo vya habari vya analojia na kwa ukosefu wa tahadhari inayoelekezwa kwake.

Zaidi ya CD 37,000 zenye sauti za mikutano ya Umoja wa Mataifa ni sehemu ya urithi wa kipekee wa sauti zilizohifadhiwa na chombo hicho. (Picha hii ni ya Januari 1948)
UN
Zaidi ya CD 37,000 zenye sauti za mikutano ya Umoja wa Mataifa ni sehemu ya urithi wa kipekee wa sauti zilizohifadhiwa na chombo hicho. (Picha hii ni ya Januari 1948)

Na kuhusu kwa nini UNESCO ikaamua kuwa na siku hii ya kumbukumbu, Bi. Azoulay anasema ni kwa ajili ya “kukuza uelewa wa umuhimu wa kutunza urithi wa sauti na picha, kusaidia taasisi zinazohusika na utunzaji wa urithi huu na kukuza uwezekano wa kuzifikia kumbukumbu hizi.”

Kwa kuzingatia umuhimu huo, amesema “UNESCO pia inahamasisha kuziweka kumbukumbu hizi katika mfumo wa kidijitali. UNESCO yenyewe imehusika kwa kiasi kikubwa katika kuhifadhi  kumbukumbu za kazi nyingi duniani kama vile matamasha ya wanamuziki nguli, marehemu Aretha Franklin na Lionel Hampton na wengineo.