Ukijifunza kwa lugha ya mama ni rahisi zaidi kuelewa- UNESCO

21 Februari 2018

Leo ni siku ya lugha ya mama duniani. Je wewe wazungumza lugha gani? Je wathamini lugha yako ya asili?

Leo ni siku ya lugha ya mama duniani ambapo Umoja wa Mataifa unasema kuwa lugha ya mama inasalia kuwa muaraboini wa kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Katika ujumbe wake wa siku hii, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO Audrey Azoulay  amesema matumizi ya lugha ya mama yanawezesha mtu au jamii kupata maarifa mapya tofauti na kupatiwa maarifa kupitia lugha isiyo ya asili kwake.

Kwa mantiki hiyo amepigia chepuo sera zinazochagiza matumizi ya lugha mama na lugha za kiasili kwenye mafunzo na maeneo ya umma akisema zinapatia uwezo jamii husika kupata maarifa mapya.

Amesema lugha ya mama ni zaidi ya mawasiliano kwa kuwa husaidia kuhamisha uzoefu, maadili na utambulisho wa  mtu pamoja na ufahamu.

Bi. Azoulay amerejelea msimamo wa UNESCO unaotaka lugha ya mama  iwe ya kwanza mtoto kufundishwa tangu mwanzo anapoanza shule.

Amesema ni vyema kutambua kuwa moja ya changamoto ya kufanikisha SDGs ni watu kutopata maarifa kwa lugha zao.

Amenukuu kauli ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela inayosema kuwa ukizungumza na mtu kwa lugha anayoelewa, jambo unalomweleza litakaa kichwani lakini ukizungumza naye kwa lugha ya mama jambo unalomweleza litakaa moyoni.

Hivyo Mkurugenzi huyo wa UNESCO ametaka serikali kusherehekea siku ya leo kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia chepuo matumizi ya lugha tofauti ambazo ndio utajiri wa dunia ya sasa.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter