Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO inatumia njia ya anga kufikisha vifaa vya matibabu kaskazini-mashariki mwa Syria.

Mtoto Ain Issa mwenye umri wa  miaka 12 akiwa na dumu la  maji baada ya safari ya siku tatu kutoka Raqqa nchini Syria.
UNICEF/Souleiman
Mtoto Ain Issa mwenye umri wa miaka 12 akiwa na dumu la maji baada ya safari ya siku tatu kutoka Raqqa nchini Syria.

WHO inatumia njia ya anga kufikisha vifaa vya matibabu kaskazini-mashariki mwa Syria.

Afya

Hii leo Shirika la afya ulimwenguni WHO limesafirisha kwa ndege zaidi ya tani 28 za dawa, vifaa vya matibabu na chanjo kwenda katika jimbo la Al-Hasakeh lililopo kaskazini-mashariki mwa Syria kwa lengo la kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya matibabu kwenye eneo hilo.

Taarifa ya WHO imesema hii ni shehena ya pili ambayo WHO imesafirisha hadi Al-Hasakeh kwa mwezi huu. Shehena ya kwanza ya tani 20 iliyokuwa na dawa ilisafirishwa kwa njia hiyo ya ndege mapema mwezi januari mwaka huu tarehe 8.

Shehena iliyosafirishwa wakati huu ina vifaa mbalimbali vya na dawa za kuweza kutibu takribani watu 106,000 na inajumuisha dawa za tiba za dharura, viuavijasumu , dawa za kuzuia sumu, dawa za magonjwa sugu na nyingine za namna mbalimbali.

Vifaa vingine ni pamoja na jenereta kwa ajili ya kuzalisha umeme, vifaa vya kutunzia Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, mashine za uangalizi wa mwenendo wa wagonjwa. Pia kuna chanjo zipatazo 140, 000 kwa ajili ya polio, kifua kikuu na hata vitamini kwa ajili ya watoto. 

WHO inasema kuwa vitu vyote vitasambazwa katika hospitali na vituo vya afya katika maeneo matatu ya kaskazini mashariki huko Al-Hasakeh, Ar-Raqqa na Deir-ez-Zor.

Mwakilishi wa WHO nchini Syria Elizabeth Hoff anasema,” maelfu ya wasyria huko kaskazini mashariki mwa Syria wana uhitaji mkubwa wa huduma ya afya. Mfumo wa afya katika maeneo yote matatu umeharibiwa sanan a hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani wanaoishi katika kambi na makazi yenye hali mbaya. Katika kuimarisha hospitali na vituo vya afya tunajikita katika kuwapatia chanjo watoto kaskazini-mashariki mwa Syria ambako viwango vya chanjo viko chini.”