Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban watu 180,000 wametawanywa na machafuko ya karibuni Syria-UNHCR

Msichana wa umri wa miaka minne akiwa kambini Bardarash huko Duhok nchini Iraq, mmoja wa maelfu wa wakimbizi ambao wamekimbia machafuko kaskazini mashariki mwa nchi yao.
© UNHCR/Hossein Fatemi
Msichana wa umri wa miaka minne akiwa kambini Bardarash huko Duhok nchini Iraq, mmoja wa maelfu wa wakimbizi ambao wamekimbia machafuko kaskazini mashariki mwa nchi yao.

Takriban watu 180,000 wametawanywa na machafuko ya karibuni Syria-UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Baada ya karibu wiki mbili za mapigano Kaskazini Magharibi mwa Syria mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yamekadiria kwamba takribani watu 180,000 wamelazimika kufungasha virako na kukimbia makazi yao , ikiwemo Watoto 80,000 na wote wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya  kuratibu masuala ya kibinadamu na msaada wa dharura OCHA leo Jumaane imearifu kwamba licha ya siku tano za usitishaji uhasama mashambulizi ya anga nan chi kavu yalianzishwa na Uturuki tarehe 9 Oktoba yakilenga maeneo yanayoshikiliwa na wakurdi upande wa pili wa mpaka yalisababisha athari kubwa kwa upande wa kibinadamu.

Kwa mujibu wa duru za Habari hii leo Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema  majeshi yake yataanza tena mashambuli isipokuwa tu kama wapiganaji wa Kikurdi wataondoka mpakani ifikapo mwisho wa siku leo.

Wakurdo ametoa askari wengi wanaopigana msitari wa mbele ambao wako katika muungano unaoendeshwa na Marekani ambao uliwafurusha ISIL kama maeneo yao katika kanda hiyo, lakini Uturuki unawachukulia wapiganaji hao kama magaidi , na ulisitisha tu mashambulizi yake kwa ombi la Marekani.

Hivi sasa mashirika ya kibinadamu yanahaha kuhakikisha watu hao wanapata huduma za msingi na kuokoa Maisha kama maji, chakula na huduma za afya. Miundombinu ya muhimu imeharibiwa mbali ya mtambo wa kusukuma maji kutofanya kazi kabisa kwa sasa vituo vine vya afya vimebomolewa na mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka kila uchao limesema shirika la OCHA.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kupitia mwakilishi wa shirika hilo nchini Syria Iman Riza linasema “ukarabai wa mfumo wa maji utaepusha janga kubwa la kibinadamu kwa wakazi wa eneo hilo kwani imemshitua sana kushuhudia hali halisi inayowakabili.”

Umoja wa Mataifa na wadau wanaongeza msaada wa kuokoa Maisha licha ya vikwazo vya kiusalama wanavyokumbana navyo. Msaada wa mablanketi na mgao wa chakula umeoangwa kuwafikia watu 580,000 raia wa majimbo ya Raqqa na Hasakeh, na juhudi zingine zinaendelea ili kutoa huduma muhimu kwa ajili ya msimu ujao wa majira ya baridi.