Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afya za waliokimbilia kambi ya Al-Hol nchini Syria mashakani, WHO yapaza sauti

Wakimbizi wakiwa kambi ya Al-Hol katika jimbo la Hasakeh kasakzini mashariki mwa Syria.
UNICEF/UN037295/Soulaiman
Wakimbizi wakiwa kambi ya Al-Hol katika jimbo la Hasakeh kasakzini mashariki mwa Syria.

Afya za waliokimbilia kambi ya Al-Hol nchini Syria mashakani, WHO yapaza sauti

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO lina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya afya kwenye kambi ya Al-Hol kwenye jimbo la Al-Hasakeh nchini Syria ambako watu wapatao 106 wengi wao wakiwa watoto wamefariki dunia kuanzia mwezi Disemba mwaka jana punde tu baada ya kufika eneo hilo au baada ya kufikishwa kwa ajili ya matibabu.

Msemaji wa WHO mjini Geneva, USwisi, Tarik Jašarević amesema sababu kubwa za vifo hivyo ni vichomi, ukosefu wa maji mwilini, utapiamlo na mwili kukosa uwezo wa kuhimili baridi kali.

“Mamia ya watu, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wanaendelea kumiminika kwenye kambi hiyo wakitokea Baghouz huko Deir-ez-Zor na sasa idadi ya watu ni zaidi ya 65,000, kiwango ambacho ni mara tano zaidi ya uwezo wa kambi hiyo, amesema Bwana Jašarević akisema wengi wao wanawasili wakiwa katika hali mbaya ya  utapiamlo uliokithiri kutokana na miaka mingi ya ukosefu wa lishe bora.

Hata hivyo amesema wafanyakazi wanaopatiwa msaada wa WHO wanafanya kazi kutwa kucha kuchunguza wanaowasili na kuwapeleka katika hospitali za ngazi ya juu zaidi iwapo inahitajika kufanya hivyo.

Mathalani watoto wenye unyafuzi wanapelekwa hospitali ya Al-Hasakeh inayopatiwa msaada na WHO ambako  hata hivyo mifumo yake ya afya inakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na kuzidiwa uwezo

Tangu tarehe 4 mwezi Disemba mwaka jana, takribani wagonjwa 500 wamepelekwa kwenye hospitali huko Al-Hasakeh.

Hospitali zikiwa zimezidiwa uwezo, wahudumu wa kibinadamu nao wanapata shida kufikia kambi hiyo ya Al-hol ambapo WHO imesihi pande husika kushughulikia haraka vikwazo hivyo.

Pamoja na wito huo, Bwana Jašarević amesema fedha za dharura zinahitajika ili kuendelea na operesheni kwenye kambi hiyo.

Katika ombi la dola bilioni 3.33 kwa ajili ya Syria mwaka huu wa 2019, dola milioni 449 ni kwa ajili ya sekta ya afya ambayo imesambaratishwa katika miaka 8 ya mzozo nchini humo, huku WHO pekee ikihitaji dola milioni 140.