'Teknolojia isilete karaha badala ya raha' Guterres aeleze jopo lake la dijitali

23 Januari 2019

Jopo la ngazi ya juu la Umoja wa Mataifa kuhusu ushirikiano wa kidijitali limetakiwa kuwa na mawazo thabiti na bunifu ya kuhakikisha kuwa teknolojia inakuwa na mchango chanya kwenye maendeleo endelevu.

Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito huo wakati jopo hilo likitamatisha mkutano wake hii leo huko Geneva, Uswisi, maendeleo ya zama za sasa za teknolojia yakijulikana pia kama mapinduzi ya nne ya viwanda  yakionekana kuleta karaha zaidi kuliko raha.

“Tafadhalini angalieni faida na hatari za zama zetu za sasa za teknolojia na kwa jinsi gani teknolojia inaweza kusaidia kufanikisha ajenda ya maendeleo endelevu, SDGs,” amesema Bwana Guterres kwa jopo hilo linaloongozwa na mfadhili Melinda Gates na mwanzilishi wa kampuni ya Alibaba Jack Ma.

Jopo hilo lilianzishwa na Katibu Mkuu Guterres mwaka 2018 likiwa na wabunifu na nguli waliobobea kwenye teknolojia akiwemo Vint Cert, mmoja wa wagunduzi wa intaneti, Sophie Eom, mgunduzi wa soko la kidijitali.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud