Guterres atiwa hofu na mapigano yaliyosababisha vifo na majeruhi Burkina Faso

5 Januari 2019

Zaidi ya raia 40 wameripotiwa kuuawa wiki hii wakati wa mapigano ya kikabila kaskazini mwa Burkina Faso hali ambayo imesababisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kutoa taarifa kulaani ghasia hizo sambamba na kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama kwenye baadhi ya maeneo ya taifa hilo la Afrika Magharibi.
 

Habari zinasema kuwa mapigano  yaliyotokea Jumatatu usiku kwenye kijiji cha Yirgou ambayo yasadikiwa kuanzishwa na watu wenye msimamo mkali ambapo mashambulizi ya kulipiza kisasi yalifanywa siku iliyofuatia dhidi ya waislamu wa kabila la Fulani ambao ni wafugaji huko wilayani Barsalogo.

Kupitia taarifa iliyotolewa mjini New York, Marekani na msemaji wake, Bwana Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na  kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi wa mapigano hayo.

Katibu Mkuu ameeleza wasiwasi wake juu ya kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama nchini Burkina Faso ambako ghasia zimeshamiri miezi ya karibuni na kusababisha serikali kutangaza hali ya hatari kwenye baadhi ya majimbo ya kaskazini yaliyoko mpakani na Mali.

Hata hivyo amesisitiza azma ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia Burkina Faso katika jitihada zake za kukabiliana na ugaidi, kuendeleza marekebisho ya sekta ya usalama, kuendeleza maridhiano ya kitaifa na kuweka mazingira endelevu ya amani na maendeleo.
 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud