Guterres alaani shambulio dhidi ya kambi ya kijeshi Burkina Faso

22 Agosti 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani shambulio la wiki hii kwenye kambi ya kijeshi ya Koutougou katika jimbo la Soum nchini Burkina Faso.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa Jumatano mjini New York, Marekani imesema shambulio hilo la tarehe 19 mwezi huu wa Agosti lilikuwa ni baya zaidi tangu kuanza kwa mwaka huu.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa askari 24 waliuawa kwenye shambulio hilo katika kambi hiyo iliyopo kaskazini mwa Burkina Faso na wengine watano walijeruhiwa katika shambulio hilo linaloelezwa kuwa linaonekana lilikuwa limepangiliwa huku ikidaiwa kuwa shambulio hilo limefanywa na magaidi.

“Natuma salamu zangu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na pia kwa wananchi wa na serikali ya Burkina Faso na pia nawatakia ahueni ya haraka majeruhi,” amesema Katibu Mkuu.

Halikadhalika amelaani mashambulio ya kiholela yanayoendelea hivi sasa dhidi ya raia akitoa wito kwa mamlaka kuhakikisha kuwa watekelezaji wa vitendo hivyo wanafikishwa haraka mbele ya sheria na kwamba, “shughuli zote za kijeshi zinafanyika kwa mujibuwa sheria za kimataifa za haki za binadamu na kibinadamu.”

Katibu Mkuu amesisitiza mshikamano na serikali na wananchi wa Burkina Faso.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud