Taarifa za kifo cha Khashoggi zimenisikitisha:Guterres 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitoa hotuba muhimu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani 10 septemba 2018
UN/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitoa hotuba muhimu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani 10 septemba 2018

Taarifa za kifo cha Khashoggi zimenisikitisha:Guterres 

Haki za binadamu

Baada ya sintofahamu ya muda leo serikali ya Saudia Arabia imethibitisha kuwa mwanahabari JamalKhashoggi aliyetoweka tangu tarehe pili Oktoba , amefariki dunia. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema amesikitishwa na taarifa hizo na anataka uchunguzi wa kina ufanyike.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema taarifa za kuthibitisha kifo cha Jamal Khashoggi zimemsikitisha sana. 
Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Ijumaa jioni , Antonio Guterres amesisitiza haja ya kufanyika uchunguzi wa kina na wa wazi kuhusu mazingira ya kifo cha mwanahabari huyo aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Saudi Arabia.

Guterres ambaye pia ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Khashoggi , jamaa na marafiki , ametaka wahusika katika kifo chake kufikishwa kwenye mkono wa sheria na kuwajibishwa.

Kwa mujibu wa duru za habari serikali ya Saudia ndio imetangaza kupitia televisheni ya taifa kuwa mwanahabari huyo wa Saudia ambaye pia alikuwa akiandika makala kwenye gazeti la Washington Post amefariki dunia ikidai ni baada ya kupigana kwenye ubalozi wa saudia mjini Instanbul Uturuki.

Khashoggi mara ya mwisho alionekana akiingia kwenye ubalozi wa Saudi Arabia mjini Instanbul Oktoba pili kwenda kuchukua nyaraka ambazo zingemruhusu kumuoa mchumba wake Hatice Cengiz.