Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2018 ulikuwa ‘tamu na chungu’ sasa tumeazimia kutokata tamaa 2019 - Guterres

Raia wa DRC akifua nguo zake katika kambi  ya wakimbizi wa ndani iliyoko milimani eneo la Masisi katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
Picha:UNHCR/S.Schulman
Raia wa DRC akifua nguo zake katika kambi ya wakimbizi wa ndani iliyoko milimani eneo la Masisi katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Mwaka 2018 ulikuwa ‘tamu na chungu’ sasa tumeazimia kutokata tamaa 2019 - Guterres

Masuala ya UM

Kuelekea mwaka mpya wa 2019, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametumia salamu zake za mwaka mpya akifanya tathmini ya mwaka 2018 na matarajio yake kwa mwaka mpya.

Mama na mwanae mchanga wakipata huduma baada ya kujifungua kwenye wodi ya wazazi iliyoko kliniki ya Shakawe nchini Botswana.
UNICEF/Christine Nesbitt
Mama na mwanae mchanga wakipata huduma baada ya kujifungua kwenye wodi ya wazazi iliyoko kliniki ya Shakawe nchini Botswana.

Katika kufanya tathmini hiyo na kutoa matarajio yake Bwana Guterres ameanza kwa kusema

Wapendwa raia wenzangu wa dunia,  Nawatakia heri ya mwaka mpya wenye furaha, amani na ustawi.”

Baada ya salamu hizo amesema kuwa wakati wa salamu zake za mwaka mpya wa 2018, alitangaza hali ya tahadhari, na kwamba hatari alizozitaja bado zipo, akisema kuwa hizi ni nyakati za wasiwasi kwa watu wengi, na dunia inapitia katika majaribu mazito.

Wakimbizi warohingya bado wanaishi wilaya ya Cox's Bazar nchini Bangladesh mwaka mmoja sasa tangu wakimbie nchi yao ya Mynamar
© UNFPA Bangladesh/Carly Learson
Wakimbizi warohingya bado wanaishi wilaya ya Cox's Bazar nchini Bangladesh mwaka mmoja sasa tangu wakimbie nchi yao ya Mynamar

Ametaja hatari hizo kuwa ni mabadiliko ya tabianchi akisema yanaenda kasi kuliko wakazi wenyewe wa dunia, migawanyiko ya kisiasa na kijiografia inazidi kuongezeka na kufanya migogoro iwe migumu kutatulika.

Halikadhalika amesema idadi kubwa ya watu wanahama kutafuta usalama na ulinzi, ukosefu wa usawa unaongezeka, na watu wanahoji dunia ambamo kwayo watu wachache wanamiliki nusu ya utajiri wa watu wote.

Kama hiyo haitoshi, “ukosefu wa stahamala unaongezeka.Uaminifu unapungua. Lakini pia kuna sababu za matumaini.  Mazungumzo ya Yemen yametengeneza fursa ya amani. Makubaliano yaliyotiwa saini mjini Riyadh mwezi Septemba kati ya Ethiopia na Eritrea yamepunguza msuguano wa muda mrefu na yameleta matarajio katika ukanda mzima. “

Guterres ametaja pia makubaliano kati ya pande kinzani kwenye mzozo wa Sudan Kusini kuwa yamechochea fursa ya amani, na kuleta maendeleo katika miezi minne iliyopita kuliko hata miaka minne iliyotangulia.

Mafuriko katika viunga vya mji mkuu wa Thailand, Bangkok miaka kadhaa iliyopita. Hivi sasa mji huo umebuni namna ya kukusanya maji chini ya ardhi na kuyatumia wakati wa ukame.
ESCAP Photo
Mafuriko katika viunga vya mji mkuu wa Thailand, Bangkok miaka kadhaa iliyopita. Hivi sasa mji huo umebuni namna ya kukusanya maji chini ya ardhi na kuyatumia wakati wa ukame.

Matumaini mengine amesema yametokana na jinsi Umoja wa Mataifa ulivyoweza kuleta nchi pamoja huko Katowice na kuridhia mpango kazi wa utekelezaji wa mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

“Sasa tunahitaji kuongeza kiwango cha matarajio yetu ili kutokomeza tishio lililopo. Ni wakati wa kutumia fursa yetu bora ya mwisho. Ni wakati wa kukomesha mabadiliko ya tabianchi yasiyodhibitika na yanayoongezeka.”

Ametaja pia mikataba miwili ya kihistoria kuhusu uhamiaji na wakimbizi, ambayo itasaidia kuokoa maisha na kukabiliana na fikra haribifu sambamba na harakati za wakazi wa dunia kuhamasishana kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Amekumbusha kuwa pindi ushirikiano wa kimataifa unapofanya kazi, dunia inashinda.

Kwa mantiki hiyo amesema katika mwaka 2019, Umoja wa Mataifa utaendelea kuleta watu pamoja kujenga madaraja na kuweka fursa za kusaka suluhu.

“Tutaendelea na shinikizo hilo. Na katu hatutokata tamaa. Na tunapoanza mwaka huu mpya, hebu na tuazimie kukabiliana na vitisho, kutetea utu wa binadamu na kujenga mustakabali bora, pamoja. Nawatakia nyote na familia zenu mwaka mpya wenye amani na ustawi.”

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.