Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2018 ulikuwa mbaya kwa watoto wanaoishi maeneo ya mizozo- UNICEF

Wanafunzi katika shule ya msingi ya mseto kati ya wakimbizi  kutoka Sudan Kusini na wenyeji nchini Uganda.
© UNHCR/Jordi Matas
Wanafunzi katika shule ya msingi ya mseto kati ya wakimbizi kutoka Sudan Kusini na wenyeji nchini Uganda.

Mwaka 2018 ulikuwa mbaya kwa watoto wanaoishi maeneo ya mizozo- UNICEF

Amani na Usalama

Mwaka 2018 ukifikia  ukingoni, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetoa tathmini ya hali ya watoto mwaka huu hususan kwenye nchi zenye mizozo na kusema ilikuwa ni mbaya kiasi cha kuweka mashakani mustakabali wao.

Mkurugenzi wa UNICEF  anayehusika na miradi ya dharura Manuel Fontaine amesema pande kinzani kwenye mizozo kuanzia Afghanistani hadi Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC bila kusahau Sudan Kusini na Somalia zimeendelea kukiuka haki za watoto wakati ambapo viongozi wa dunia wanashindwa kuwawajibisha watekelezaji wa vitendo hivyo.

“Watoto wanaoishi kwenye nchi zenye mizozo wameshambuliwa moja kwa moja, wametumiwa kama ngao vitani, wameuawa, wameachwa na ulemavu au wametumikishwa vitani. Ubakaji, ndoa za lazima na utekwaji vimekumba mbinu za kawaida kwenye mizozo kuanzia Syria, Yemen, DRC, Nigeria, Sudan Kusini hadi Myanmar,” amesema Bwana Fontaine.

Mathalani amesema huko DRC, mapigano ya kikabila pamoja na mapigano kati ya jeshi la serikali na vikundi vilivyojihami kwenye eneo la Kasai Kuu, jimbo la Tanganyika, Ituri, Kivu Kusini na Kivu Kaskazini, yamekuwa na madhara makubwa kwa watoto. Takribani watoto milioni 4.2 wako hatarini kukumbwa na unyafuzi.

Mtoto huyu mwenye umri wa miaka 6 kutoka kabila la warohingya  nchini Myanmar, sasa anaishi kambini Bangladesh. Baba  yake anasema walilazimika kukimbia baada ya askari kuvamia nyumba yao na kumpiga mwanae huyu pindi alipokataa kuwaeleza alipo baba yake.
© UNICEF/Thomas Nybo
Mtoto huyu mwenye umri wa miaka 6 kutoka kabila la warohingya nchini Myanmar, sasa anaishi kambini Bangladesh. Baba yake anasema walilazimika kukimbia baada ya askari kuvamia nyumba yao na kumpiga mwanae huyu pindi alipokataa kuwaeleza alipo baba yake.

Huko nchini Sudan Kusini, amesema mzozo na ukosefu wa usalama wakati wa mwaka mzima wa mwambo umeweka watu milioni 6.1 kwenye njaa kali na kwamba  licha ya mkataba mpya wa amani kuleta matumaini, bado ukatili dhidi ya wanawake na watoto umeshamiri akitolea mfano tukio la hivi karibuni huko Bentiu ambako zaidi ya wanawake na wasichana 150 walibakwa.

Mkurugenzi huyo wa UNICEF amesema ingawa mkataba wa haki za mtoto duniani, CRC ukitimiza miaka 30 mwaka 2019, bado kuna nchi zipo kwenye mizozo ya ndani au ya kimataifa kuliko wakati wowote ule kwenye miongo mitatu iliyopita.

Amesema “UNICEF imetoa wito kwa pande kinzani kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu na kukomesha ukiukwaji wowote wa haki dhidi ya watoto, sambamba na kushawishi pande kinzani kuacha kutumia watoto  kama ngao kwenye mapigano.”

Hata hivyo amesema UNICEF katika nchi hizo zenye mizozo inaendelea kufanya kazi na wadau ili kuhakikisha watoto walio hatarini wanapata huduma za msingi kama vile elimu, lishe na ulinzi.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.