Visa vya kigaidi mjini Tripoli havivumiliki:UNSMIL

26 Disemba 2018

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL umelaani shambulio la kigaidi  lililofanywa jana kwenye ofisi za wizara ya mambo  ya nje nchini humo kwenye mji mkuu Tripoli.

Hadi sasa hakuna taarifa ya kundi gani lilihusika shambulio hilo wala idadi ya watu waliouawa au kujeruhiwa.

Taarifa ya UNSMIL iliyotolewa mjini Tripoli, Libya imesema ujumbe huo pamoja na kulaani shambulio hilo pia umetuma salamu za rambirambi kwa ndugu na jamaa za waathirika wa shambulio hilo na kukariri kuwa shambulio dhidi ya taasisi ni shambulio dhidi ya wananchi wote wa Libya.

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya,Ghassan Salame, amenukuliwa kwenye taarifa hiyo ya UNSMIL akisema kuwa , ‘kamwe ugaidi hautafaulu dhidi ya uamuzi wa watu wa Libya wa kusonga mbele kujenga  taifa lao na pia kupinga machafuko.Hatutakubali shambulio lolote dhidi ya taasisi, hususan shambulio ambalo limefanywa na kundi la kigaidi. Tutashirikiana na watu wa Libya kuzuia makundi ya kigaidi dhidi ya kuifanya Libya kuwa uwanja wa fujo na kutenda makosa.”

Kufuatia shambulio hilo, Bwana Salame ambaye  pia ni mkuu wa UNSMIL aliwasiliana na serikali kuu na kulaani visa vya kigaidi, na vilevile kutoa salamu zake za rambirambi na kuomba kuimarisha ulinzi wa taasisi za umma.

UNSMIL imesema kwa ushirikiano na uongozi wa Tripoli, inafuatilia hatua za kuchukuwa kufuatia shambulio hilo na iko tayari kusaidia.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter