UNSMIL yalaani vikali shambulio dhidi ya Chuo Cha Kijeshi, Hadaba, Libya

5 Januari 2020

Watu kadhaa wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa kutokana na shambulizi la anga lililolenga Chuo cha kijeshi huko Hadaba, kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Katika taarifa iliyotolewa hii leo jumapili na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL, imelaani vikali mashambulizi hayo ya mabomu yaliyotekelezwa jumamosi katika chuo cha kijeshi, tukio ambalo kwa mujibu wa vyombo vya habari limewaua watu 30 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 30.

Sehemu ya taarifa hiyo imeeleza, “kuongezeka kwa mashambulizi haya ya kijeshi kuna kunaivuruga zaidi hali nchini Libya na kunatishia uwezekano wa kurejea katika mchakato wa mazungumzo ya kisiasa.”

Pia taarifa ya UNSMIL imekumbusha kuwa, “kuendelea kwa mashambulizi ya mabomu katika makazi ya raia na vituo vya huduma za kiraia kama vile hospitali na shule, kunaweza kuongeza uhalifu wa kivita na watekelezaji hawatakwepa kuadhibiwa.”

UNSMIL imetuma salamu zake za rambirambi huku ikiwatakia kupona haraka wale wote waliojeruhiwa.

Wakati huo huo, wizara ya mambo ya nje ya Libya imeitisha kikao cha dharura cha Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ili kujadili suala hilo ikisema, “Jenerali Haftar anatakiwa kuchunguzwa na mahakama ya uhalifu wa kivita ICC kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.”

Jenerali Haftar anatuhumiwa kuiasi serikali na kujiunga na upande unaoipinga serikali ya Libya.

Usaidizi wa kijeshi kutoka nje utachochea mgogoro

Wakati haya yakijiri, juzi alhamís, bunge la Uturuki lilipiga kura ya kuruhusu majeshi yake kwenda Libya kuisaidia serikali jambo ambalo taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ilieleza kuwa linaweza kuchochea mgogoro na kuhatarisha mchakato wa mazungumzo ya kisiasa kuelekea amani ya Libya.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter