Skip to main content

Shambulio nchini Libya linaweza kuwa uhalifu wa kivita- Salamé

Matokeo ya shambulio la kituo cha kizuizini cha Tajoura mjini Tripoli, Libya Julai 2.
IOM/Moad Laswed
Matokeo ya shambulio la kituo cha kizuizini cha Tajoura mjini Tripoli, Libya Julai 2.

Shambulio nchini Libya linaweza kuwa uhalifu wa kivita- Salamé

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa na mashirika yake umelaani vikali shambulio la jana  kwenye mji mkuu wa Libya Tripoli ambalo limesababisha vifo vya takribani watu 44 na wengine zaidi ya 130 wamejeruhiwa.

Shambulio hilo lilifanyika kwenye eneo la Tajoura ambamo wanashikiliwa wahamiaji ambapo ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL umelaani vikali ukisema kuwa hii ni mara ya pili eneo hilo linalohifadhi zaidi ya wahamiaji 600 linashambuliwa.

Guterres apaza sauti

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pamoja na kutuma salamu za rambirambi kwa wafiwa na kuwahatia ahueni ya haraka majeruhi, ametaka uchunguzi wa kina na huru ufanyike juu ya mazingira ya shambulio hilo ili wahusika wafikishwe mbele ya sheria kwa sababu, “Umoja wa Mataifa uliwasilisha kwa pande husika kwenye mzozo huo, taarifa sahihi kuhusu eneo lilipo kituo hicho cha kushikilia wahamiaji na wakimbizi.”

Majengo yakiwa yamesalia mapagala na magofu baada ya mashambulizi yanayoendelea huko Tripoli nchini Libya
OCHA/Giles Clarke
Majengo yakiwa yamesalia mapagala na magofu baada ya mashambulizi yanayoendelea huko Tripoli nchini Libya

Katibu Mkuu amekumbusha pia pande zote wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu akitaka pande hizo zitumie tahadhari zote kukwepa au kupunguza katika tukio lolote lile mauaji ya raia au uharibifu wa miundombinu ya raia pamoja na kuepuka kushambulia raia.”

Ameongeza kuwa tukio la jana usiku linapatia msisitizo umuhimu wa kuwapatia haraka wahamiaji na wakimbizi makazi salama hadi pale maombi yao ya hifadhi yatakapokamilika na waweze kusafirishwa.

Halikadhalika Bwana Guterres amesisitiza wito wake wa kutaka kukoma kwa mapigano ili mazungumzo ya kisiasa yaweza kuanza tena.

Mkuu wa UNSMIL naye azungumza

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Ghassan Salamé, amesema shambulio hilo linaweza kuwa uhalifu wa kivita, kwa kuwa limesababisha mauaji ya raia wasio na hatia na ambao mazingira yao magumu yamesababisha waishi kwenye eneo hilo.

Amesema mapigano yasiyo na maana yanayoendelea Libya yamesababisha ukatili na madhara makubwa akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kulaani uhalifu huo na kusaka adhabu kali dhidi ya wale walioagiza, waliotekeleza na wanaosambaza silaha na kukiuka sheria za kimataifa za kibinadamu.

IOM na UNHCR nazo zapaza sauti

Wakati huo huo, mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la uhamiaji na lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR yametoa taarifa yao ya pamoja yakisema kuwa shambulio hili la karibuni zaidi ni ishara ya janga linalokumba wahamiaji na wakimbizi wanaorejeshwa Libya baada ya kukamatwa au kuokolewa bahari ya Mediteranea.

Wahamiaji watoto wakitembea nje ya kizuizi mjini Tripoli, Libya
UNICEF/Romenzi
Wahamiaji watoto wakitembea nje ya kizuizi mjini Tripoli, Libya

Mashirika hayo yamelaani shambulio hilo yakitoa wito wa kukoma mara moja kwa kitendo cha wahamiaji na wakimbizi kuswekwa korokoroni na kwamba ni lazima makundi hayo yalindwe.

Halikadhalika wamesema shambulio hilio linahitaji zaidi ya kulaani na hivyo yamesema yanaamini kuwa uchunguzi huru na wa haki unahitajika ili kubaini kile kilichotokea na nani anahusika ili waweze kufikishwa mbele ya sheria.

Kando mwa manusura wa shambulio la Tajoura, bado mjini Tripoli wahamiaji wapatao 3,300 wanashikiliwa kiholela na katika mazingira duni hivyo mashirika hayo yametaka vituo hivyo vifungwe.

Kinachofanyika sasa huko Tajoura

UNHCR na IOM wanasema tayari wamepeleka timu za wahudumu wa afya ilihali timu nzima ya pamoja ya Umoja wa Mataifa ikisubiri ruhusa ya kuingia eneo la shambulio.

Mzozo unaoendelea mjini Tripoli umelazimisha raia wapatao 100,000 kukimbia makazi yao huku UNHCR na wadau wake ikiwemo IOM wakihamisha zaidi ya wakimbizi 1,500 kutoka maeneo hatari ili kwenda meneo salama zaidi.

Mwaka huu pekee, IOM kupitia mradi wake wa kurejesha wahamiaji na wakimbizi nyumbani kwa hiari, imesaidia zaidi ya watu 5,000 waliokuwa hatarini kurejea katika mataifa 30 ikiwemo ya Afrika na Asia.

Daktari katika matibabu ya mtoto wa umri wa miaka minne nchini Libya ambapo yaelezwa kuwa mzozo ukiendelea hosptiali zinakabiliwa na mzigo mkubwa.
WHO
Daktari katika matibabu ya mtoto wa umri wa miaka minne nchini Libya ambapo yaelezwa kuwa mzozo ukiendelea hosptiali zinakabiliwa na mzigo mkubwa.

Pande kinzani zilikuwa na taarifa ya uwepo wa eneo hilo, kwa nini mashambulizi?- Bachelet

“Nimeshtushwa na vifo na majeruhi ya makumi ya wahamiaji na wakimbizi kwenye kituo cha kushikilia watu huko Tajoura, ambacho kimeripotiwa kushambuliwa kwa kombora la kutoka angani Jumanne, usiku,” amesema Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet kufuatia shambulio hilo la jana.

Kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi yake, Bi. Bachelet amesema suala kwamba mawasiliano kuhusu eneo lilipo kituo hicho na taarifa ya kwamba linahifadhi raia  yalifikishwa kwa pande kwenye mzozo wa Libya, ni dhahiri kuwa shambulio ambalo limefanyika kwa uhakika, linaweza kuwa uhalifu wa kivita.

Amesema kwamba pande kinzani kwenye mzozo zinapaswa kulinda raia na miundbombinu kama vile shule na hospitali na kwamba misingi ya kutenganisha, uwiano na tahadhari inapaswa kuzingatiwa kila wakati, ikiwemo kuepusha kufuatilia vifaa vya kijeshi vilivyopo karibu na maeneo ya raia.

“Kila mara nimetoa wito wa kufungw kwa vituo vinavyoshikilia wahamiaji na wakimbizi nchini Libya, ambako wafanyakazi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamefuatilia na kubaini mateso, utumikishwaji, ubakaji na utapiamlo uliokithiri,” amesema Bachelet.

Halikadhalika amesema kila wakati ametaka kuachiliwa hur kwa wahamiaji hao na wakimbizi na waruhusiwe kupatiwa uhifadhi wa kibinadamu, na makazi ya pamoja ambayo ni salama kutoka maeneo ya mapigano.