Pande kinzani Yemen heshimuni makubaliano kuhusu Hudaidah- Baraza

21 Disemba 2018

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limeridhia kwa kauli moja makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya Yemen na wapiganaji wa kihouthi, wakati wa mashauriano yao nchini Sweden wiki iliyopita.

Rasimu ya azimio la kupitisha makubaliano hayo iliandaliwa na Uingereza ambapo baraza pia limeridhia kupelekwa kwa jopo la kuwezesha ufuatiliaji na utekelezaji wa makubaliano ya Stockholm.

Kupitia azimio hilo namba 2451 la mwaka huu wa 2018, Baraza linasisitiza kuwa, “pande zote zinapaswa kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano kwenye jimbo la Hudaidah pamoja na ahadi zao za kuondoa vikosi vyao kwenye mji wa bandari wa Hudaidah na kupeleka kwenye maeneo yaliyokubaliwa nje ya mji katika kipindi cha siku 21 tangu mkataba huo utakapoanza kutekelezwa.”

Nyumba zilizobomolewa kwa makombora kutoka angani kwenye mji mkuu wa Yemen, Sana'a.
OCHA/Charlotte Cans
Nyumba zilizobomolewa kwa makombora kutoka angani kwenye mji mkuu wa Yemen, Sana'a.

Vipengele vingine kwenye azimio hilo ni kwamba pande zote zifanye kazi kwa ufanisi na kwa nia njema bila masharti yoyote na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Martin Griffiths, ikiwemo kufanya kazi kukwamua uchumi kwenye taifa hilo lililogubikwa na vita tangu mwaka 2015 sambamba na kusaka njia za kufungua tena uwanja wa ndege wa Sana’a na kurejea meza ya mazungumzo mwezi Januari mwakani kama walivyokubaliana.

Kupitia azimio hilo pia, Baraza la Usalama limempatia mamlaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuunda na kupeleka kwa kipindi cha siku 30, jopo tangulizi la kuwezesha na ufuatiliaji wa mkataba wa Stockholm.

Wajumbe pia wameeleza masikitiko yao kutokana na kuendelea kwa matukio ya vifo miongoni mwa raia nchini Yemen wakilaani kitendo cha matumizi ya watoto kwenye uwanja wa vita na kusisitiza kuwa wote wanaopigana vita nchini humo lazima wahakikishe raia wanalindwa na wanaruhusiwa kukimbilia maeneo salama.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter