Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taswira ya Yemen 2018 ilikuwa ya kutisha lakini kuna nuru 2019- Griffiths

Bandari ya Hudaydah nchini Yemen ni moja ya njia muhimu kwa ajili ya kuwasilisha misaada nchini Yemen.
UN OCHA/GILES CLARKE
Bandari ya Hudaydah nchini Yemen ni moja ya njia muhimu kwa ajili ya kuwasilisha misaada nchini Yemen.

Taswira ya Yemen 2018 ilikuwa ya kutisha lakini kuna nuru 2019- Griffiths

Amani na Usalama

Mwaka 2018 umekuwa mwaka wa 'kutisha' kwa wananchi wa Yemen lakini hata hivyo  unamalizika kwa matumaini kufuatia mazungumzo ya mwezi huu huko Sweden.

Hiyo ni kauli ya Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Martin Griffiths aliyotoa wakati wa mahojiano maalum kwa njia ya simu na Idhaa ya kiarabu ya umoja huo kutoka Amman, Jordan.

Bwana Griffiths ametaja matumaini hayo kuwa ni makubaliano ya sitisho la mapigano kwenye mji wa bandari wa Hudaidah, ambayo yameenda sambamba na mwitikio wa pande kinzani wa kufanyika kwa mashauriano zaidi mwezi ujao.

Hata hivyo ameseama licha ya mafanikio hayo ya hivi karibuni, bado Yemen inaendelea kukabiliwa na janga la kibinadamu ambalo tayari Umoja wa Mataifa umelielezea kuwa ni janga baya zaidi kuliko majanga yoyote ya kibinadamu duniani hivi sasa.

Amesema mapigano yanayoendelea kati ya serikali na wahouthi nchini Yemen yatakwamisha baadhi ya harakati za amani.

Jukumu la Umoja wa Mataifa

Kwa mujibu wa mjumbe huyo maalum, Umoja wa Mataifa ni chombo pekee ambacho kinaweza kufanikisha makubaliano kama sitisho la mapigano Hudaidah pamoja na kufanikisha pande kinzani kuwepo kwa wiki nzima kwa ajili ya mashauriano huko Sweden.

“Bila shaka kuelekea kuanza kwa mashauriano hayo tarehe 6 mwezi Desemba, kulikuwepo na shaka na shuku, lakini pia hisia za mafanikio kwa kuweza tu kuweka pandeo zote kinzani pamoja kwenye chumba kimoja, baada ya miaka ya vita, ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo baada ya miaka mwili,” amesema Bwana Griffiths akionyesha dhima muhimu ya Umoja wa Mataifa katika mchakato wa amani Yemen.

Amesisitiza pia umuhimu wa kutumia mikutano tangulizi ili kusongesha usimamizi wa Hudaidah kufuatia mkataba tete wa sitisho la mapigano kwenye bandari hiyo muhimu inayotumika kuingiza shehena za kibinadamu pamoja na kibiashara.

Kuhusu usaidizi wa kibinadamu, mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen amesema mpango wa kina unaandaliwa na ofisi ya mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa Yemen, Lise Grande pamoja na shirika la mpango wa chakula duniani, WFP, ambapo WFP itakuwa na dhima ongozi katika usimamizi wa bandari ya Hudaidah.

Vijana wa Yemen wakiwa wamekalia magodoro waliyopewa na UNHCR Sirwan, Yemen. Zaidi ya milioni mbili wamesambatishwa na mapigano ya Yemen.
MDF/M. Hudair
Vijana wa Yemen wakiwa wamekalia magodoro waliyopewa na UNHCR Sirwan, Yemen. Zaidi ya milioni mbili wamesambatishwa na mapigano ya Yemen.

Kubadilishana wafungwa

Suala lingine ambalo ametaja kuwa ni mafanikio makubwa kutokana na mashauriano ya Sweden ni makubaliano ya kubadilishana wafungwa yakihusisha jumla ya wafungwa 4,000, (wafungwa 2,000) kutoka kila upande.

“Wafungwa hao sasa watarejea nyumbani na itakuwa ni wakati wa kipekee kwa familia na ni ishara muhimu mno kwa ya matumaini kwa wananchi wa Yemen,” amesema Bwana Griffiths.

Ameongeza kuwa kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu, ICRCR ilikuwepo kwenye mashauriano nchini Sweden na imekubali kusimamia usafirishaji wa wafungwa hao kwa njia ya anga kutoka sehemu moja ya Yemen kwenda sehemu nyingine ya nchi hiyo.

Dhima ya vikundi vya wanawake

Akigusia pia harakati nyingine ambazo mara nyingi hazionekani lakini ni kichocheo kikubwa cha amani, Yemen, Bwana Griffiths ametaja kikundi cha ushauri wa kiufundi cha wanawake wa Yemen ambacho amesema wakati wa mashauriano nchini Sweden, kilikuwa na mashauriano na pande zote mbili kwenye mzozo wa Yemen.

“Kikundi hicho  kilijadili jinsi ya kujumuisha sauti za wanawake wa Yemen kwenye mchakato wa amani na kiliwasilsiha nyaraka za mkakati na mapendekezo yatakayomwongoza mjumbe maalum kwenye dhima yake ya usuluhishi ili kumaliza vita.

Masuala ambayo bado yanahitaji kushughulikiwa

Bwana Griffiths, ametaja masuala mawili ambayo pande kinzani yalishindwa kufikia muafaka nchini Sweden ambayo ni kufunguliwa kwa bandari ya Sana’a na Benki Kuu ya Yemen kukusanya mapato.

Kuhusu bandari ya Sana’a Bwana Griffiths amesema ufunguzi wa bandari hiyo bado majadiliano yanaendelea na suala hilo linapaswa kupatiwa ufumbuzi kabla ya mashauriano mwezi ujao.

“Ni matumain ikwamba wataalamu kutoka Benki Kuu kwa usaidizi kutoka shirika la fedha duniani, IMF, wataweza kuandaa mchakato wa wazi wa ukusanyaji mapato ili wafanyakazi wa umma nchini Yemen ambao kwa miezi kadhaa hawapata mishahara, waweze kulipwa mishahara yao,” ameseme mjumbe huyo.

Hata hivyo amesema la msingi ni kwamba mwaka huu unavyotamatishwa, maoni ya jamii ya kimataifa kuhusu Yemen yamekuwa dhahiri na hivyo kuongeza matumaini ya kumalizwa kwa mzozo mwakani 2019.

“Kwa kuangalia mbele, nina matumaini kuwa awamu ijayo ya mashauriano itajadili mambo mengi zaidi ya masuala ya kibinadamu, kwa kuanza kushughulikia mambo muhimu ya suluhisho la kisiasa kwenye mzozo wa yemen,” ametamatisha Griffiths.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.