Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres asihi pande kinzani Yemen zitekeleze makubaliano yao ya Sweden

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kati) akiwa na Waziri wa Mambo ya nje wa Sweden, Margot Wallström (kulia kwake) na Martin Griffiths na wawakilishi wa pande kinzani kutoka Yemen leo tarehe 13 Desemba 2018
Serikali ya Sweden/Ninni Andersson
Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kati) akiwa na Waziri wa Mambo ya nje wa Sweden, Margot Wallström (kulia kwake) na Martin Griffiths na wawakilishi wa pande kinzani kutoka Yemen leo tarehe 13 Desemba 2018

Guterres asihi pande kinzani Yemen zitekeleze makubaliano yao ya Sweden

Amani na Usalama

Mashauriano kati ya pande kinzani nchini Yemen yakikunja jamvi hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesihi wajumbe hao kuhakikisha kuwa makubaliano waliyofikia yanatekelezwa ili hatimaye kumaliza miaka minne ya machungu ambayo wayemen wamekabiliana nayo.

Akihutubia wajumbe hao mwishoni mwa kikao hicho cha mashauriano huko Rimbo nchini Sweden Bwana Guterres amesema utekelezaji wa makubaliano hayo ni jambo muafaka kwa kuzingatia kuwa janga la Yemen, ni janga baya zaidi la kibinadmau likisababisha robo tatu ya wakazi wa nchi hiyo kuhitaji misaada ya kibinadamu ili waweze kuishi.

Ametaja makubaliano hayo kuwa ni pamoja na hatma ya mji wa bandari wa Hudaydah ambapo sasa kila upande utapeleka vikosi vyake na kuwepo kwa sitisho la mapigano jimboni kote badala ya hali ya sasa ya mji huo kuwa chini ya udhibiti wa wahouthi. 

Halikadhalika ametaja pia mji wa Taizz akisema “mmekubaliana kulegeza hali ilivyo mjini Taizz. Natumai hii itawezesha kufungua milango kwa wahudumu wa kibinadamu kufikisha misaada pamoja na kufanyika kwa kazi ya kutegua mabomu.”

Mkutano wa mashauriano kuhusu Yemen ukifanyika nchini Sweden
Ninni Andersson/Government Offices of Sweden
Mkutano wa mashauriano kuhusu Yemen ukifanyika nchini Sweden

Guterres pia ametaja makubaliano kati ya pande hizo mbili aliyosema ni hatua muhimu kuliko zote inayohusu mchakato wa amani akisema. “mmekubaliana kushiriki zaidi katika majadiliano ya mfumo wa mashauriano katika kikao kijacho. Hiki ni kipengele muhimu kwa mustakabali wa kusaka suluhu ya kisiasa na kumaliza mzozo.”

Pande zimekubaliana kukutana tena kujadili suala hilo mwishoni mwa mwezi januari mwakani. “Lakini kati ya sasa na mwezi Januari, tutakuwepo wakati wowote kuendelea kujadili na kujaribu kusongesha mbele masuala ambayo bado hayajaguswa kwenye majadiliano na mkataba,” amesema Katibu Mkuu.

Amewakumbusha wajumbe hao ambao wamekutana Rimbo kuanzia tarehe 6 mwezi huu wa Desemba kuwa “kile mlichokubaliana hapa kitakuwa na maana kubwa kwa mustakabali wa wananchi wa Yemen. Kitakuwa na maana kubwa kwa wayemen ambao wataona matokeo thabiti katika maisha yao ya kila siku.”

Mashauriano hayo yaliongozwa na Umoja wa Mataifa chini ya mjumbe wake maalum Martin Griffiths huku mwenyeji Sweden nayo ikihakikisha mazingira ya mkutano yalikuwa muafaka kwa kikao hicho ambapo Katibu Mkuu ameshukuru wenyeji Sweden sambamba na mataifa yote yaliyowezesha kufanyika kwa mashauriano hayo ya kwanza kabisa ya uso kwa uso kati ya wahouthi na wawakilishi wa serikali  ya Yemen  tangu miaka miwili iliyopita.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.